Mradi wa ujenzi wa uwanja wa Arusha umefikia asilimia 23 ambapo ni miezi nane tu tangu kuanza kwa ujenzi huo unaotarajiwa kukamilika katika kipindi cha miaka miwili.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Utawala na usimamizi wa rasilimali watu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo bi. Savera salvatory alipokuwa kwenye ziara ya kutembelea mradi huo pamoja na baadhi ya watumishi wa wizara hiyo leo Februari Mosi 2025 jijini Arusha.
Aidha, Bi. Savera amemshukuru Mhe. Rais kwa kuendeleza sekta ya michezo na viongozi wa Wizara hiyo kwa kuhakikisha miradi mbalimbali inaendelea kama inavyopangwa.
Katika hatua nyingine, mmoja wa watumishi hao waliotembelea mradi huo amewashukuru viongozi wa Wizara hiyo kwa kuwapa nafasi ya kutembelea na kujionea maendeleo ya mradi huo.
Naye Meneja wa mradi huo Bw. Dennis Benito amebainisha kuwa sambamba na uwanja wa mpira, kutakuwa na maeneo mengine kama vile kumbi za mikutano, uwanja wa mpira wa kikapu, eneo la kina mama kunyonyesha pamoja na viwanja vya mazoezi.
Sambamba na hilo, Watumishi hao walishiriki mazoezi na kikosi cha kamati ya usalama mkoa wa Arusha ambapo walijumuika kwenye mazoezi ya pamoja na baadaye waliungana na watoto wa kituo cha Kindness kilichopo eneo la Kijenge jijini humo na kutoa mahitaji mbalimbali kwa watoto hao.