Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anatarajiwa kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump na ajenda ya kuzingatia vita vilivyositishwa huko Gaza, pamoja na Iran.
Viongozi hao wawili wanatarajiwa kukutana mapema alasiri siku ya Jumanne, vyanzo viliambia mashirika ya habari. Mkutano huo unafanyika wakati mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Israel na Hamas inayoungwa mkono na Iran kuhusu awamu ya pili ya makubaliano ya kusitisha mapigano Gaza yanatarajiwa.
Kabla ya mkutano huo, Trump alisema kuwa majadiliano na Israel na nchi nyingine kuhusu Mashariki ya Kati “yanaendelea” lakini hakutoa maelezo yoyote.
Kiongozi huyo wa Marekani alikiri, hata hivyo, kwamba usitishaji mapigano hauna uhakika. “Sina hakikisho kwamba amani itaendelea,” aliwaambia waandishi wa habari.
Mjumbe wake wa Mashariki ya Kati Steve Witkoff, ambaye alikutana na kiongozi wa Israel siku ya Jumatatu, aliongeza: “Hakika tuna matumaini.”
Ofisi ya Netanyahu ilitangaza Jumanne kwamba timu ya mazungumzo ya Israeli inajiandaa kusafiri hadi Qatar wikendi hii kwa mazungumzo ya awamu ya pili. Timu hiyo itajadili “maelezo ya kiufundi kuhusiana na kuendelea kutekeleza” makubaliano, ilisema katika taarifa.