Kiongozi mkuu wa vuguvugu la Hezbollah la Lebanon alisema Jumapili kwamba mtangulizi wake, Hassan Nasrallah, atazikwa tarehe 23 Februari, karibu miezi mitano baada ya kuuawa katika shambulio la anga la Israel kwenye viunga vya kusini mwa Beirut, Reuters imeripoti.
Nasrallah aliwahi kuwa katibu mkuu wa Hezbollah kwa zaidi ya miaka 30. Aliuawa tarehe 27 Septemba wakati Israeli ilipoongeza mashambulizi yake ya anga kwenye maeneo ya Hezbollah siku chache kabla ya wanajeshi wa Israel kuanza mashambulizi ya ardhini kusini mwa Lebanon.
Mrithi wake Naim Qassem alisema katika hotuba ya televisheni siku ya Jumapili kwamba Nasrallah aliuawa “wakati ambapo hali ilikuwa ngumu,” na kulazimisha vuguvugu hilo kufanya mazishi ya muda kwa ajili yake kulingana na utamaduni wa kidini.
Qassem alisema kuwa harakati hiyo sasa imeamua kufanya “maandamano makubwa ya mazishi yenye hadhara kubwa” kwa Nasrallah na Hashem Safieddine, afisa mwingine wa ngazi ya juu wa Hezbollah aliyeuawa katika shambulio la anga la Israel karibu wiki moja baada ya Nasrallah.
Ilithibitishwa na Qassem kwa mara ya kwanza kwamba Safieddine alikuwa amechaguliwa kama mrithi wa Nasrallah lakini aliuawa kabla ya uteuzi huo kuwekwa wazi.
Alisema Safieddine pia atazikwa kwa cheo cha katibu mkuu.