Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali, kwa kuwanoa wataalam kutoka katikaTaasisi zake kwa ajili ya maandalizi ya daftari la huduma za Serikali na kuifanya kuwa Wizara ya kwanza kujinoa kwa zoezi hilo.
Akifungua kikao kazi cha maandalizi ya daftari la kieletroniki la huduma za serikali, kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimali watu Serikalini, SACP. Ibrahim Mahumi, licha ya kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua hiyo muhimu, amesema kuwa daftari hilo litakuwa chachu ya kuboresha utoaji wa huduma katika Taasisi za Wizara hiyo.
SACP. Mahumi amesema kuwa kwa kutambua umuhimu wa kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa mwananchi, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR – MUUUB) inaandaa Daftari la Kielektroniki la Huduma za Serikali kwa Taasisi zote za Serikali kwa lengo la kuwawezesha wananchi, wafanyabiashara, watumishi wa umma na taasisi mbalimbali za Serikali kupata taarifa za huduma zote zinazotolewa na Taasisi za Serikali kwenye chanzo kimoja.
“Naipongeza Menejimenti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kulipa umuhimu suala hili na kuwezesha kukutana kwa Taasisi zote zilizo chini yenu ili kukamilisha zoezi la kuandaa Daftari la Huduma za Serikali”. Aliongeza SACP. Mahumi