Umoja wa Ulaya umelaani marufuku ya serikali ya Israel inayokalia kwa mabavu dhidi ya shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina katika Mashariki ya Karibu (UNRWA), tovuti ya habari ya Wafa ya Palestina imeripoti.
Katika taarifa iliyotolewa Jumapili, Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Ulaya kwa Masuala ya Kigeni na Sera ya Usalama Kaya Kallas alisema sheria ya Israel inazua wasiwasi kutokana na athari zake za kina kwa operesheni za UNRWA katika Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, na Gaza.
Taarifa hiyo ilionyesha kuwa EU inalaani majaribio yoyote ya “kufuta makubaliano ya 1967 kati ya Israeli na UNRWA au kujaribu kuzuia uwezo wa UNRWA kutekeleza majukumu yake.”
“EU inasisitiza jukumu la Umoja wa Mataifa na mashirika yake, hasa UNRWA, ambayo inatoa msaada muhimu kwa wakazi wa Gaza, Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem mashariki, na katika eneo zima, ikiwa ni pamoja na Lebanon, Syria na Jordan. Utoaji wa huduma muhimu kwa wakimbizi wa Kipalestina ni muhimu zaidi sasa wakati kuna haja ya utekelezaji wa haraka wa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuwaachilia mateka.