Naibu Waziri wa Nishati, Mhe Judith Kapinga amesema kuwa hadi kufikia Januari, 2025, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imekamilisha upelekaji wa umeme kwenye vijiji vyote 12,318 nchini na kwamba kazi inayofanyika sasa ni kuendelea kusambaza umeme vitongojini.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Februari 04, 2025 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la la Mbunge wa Viti Maalumu Mhe. Jacquelune Andrew aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itamaliza kusambaza umeme kwenye Vitongoji nchini.
“Serikali imepeleka umeme kwenye vitongoji 33,657 kati ya vitongoji 64,359 sawa na asilimia 52.3”, Amesema Mhe. Kapinga
Ameongeza kuwa, Vitongoji 30,702 vilivyobaki vitapata umeme kupitia mpango wa miradi ya kusambaza umeme katika vitongoji ambapo tayari Serikali imeshaandaa Mpango wa kupeleka umeme katika vitongoji 20,000 kwa kipindi cha kati ya miaka mitano (5) hadi kumi (10) kuanzia Mwaka wa Fedha 2023/24.
Mhe. Kapinga ameongeza kuwa, vitongoji 4,020 tayari vipo katika Mpango wa utekelezaji kupitia miradi mbalimbali.
Akijibu swali la Mbunge wa Kilindi, Mhe. Omar Kigua aliyeuliza ni upi mpango wa Serikali kufikisha umeme kwenye maeneo yote ya uchimbaji wa madini Kilindi, Mhe. Kapinga amesema Wilaya ya Kilindi ina maeneo yapatayo 12 ya uchimbaji wa madini ya dhahabu ambapo kati ya hayo, maeneo 4 tayari yameshapatiwa huduma ya umeme.
Ameyataja maeneo yenye umeme kuwa Maeneo ni Mafulila, Mfyalime/Najim, Masagulu Muheza na Chanungu. Aidha, eneo la Matanda, mkandarasi aitwae DIEYNEM Co. Ltd anaendelea na kazi ya kuweka miundombinu ya umeme na anatarajia kukamilisha kazi hiyo hivi karibuni.
Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa maeneo mengine ya migodi yaliyosalia yatapata umeme kupitia miradi mbalimbali itakayofuata.
Kuhusu utekelezaji wa mradi wa gridi imara katika maeneo ya Mkata na Kilindi Mhe. Kapinga amesema wanaendelea na mazungumzo na Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupeleka fedha za kutekeleza mradi huo.