Katibu tawala wilaya ya Geita , Lucy Beda amewaelekeza waratibu wa Chanjo pamoja na watendaji wa kata kuhakikisha wanapeleka elimu ya chanjo Mashuleni pamoja ili wanafunzi waweze kuelewa na kuchukua hatua.
Maelekezo hayo ameyatoa katika Kikao cha Tathimini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe Robo ya Pili kwa Mwaka wa Fedha 2024 – 2025 Octoba na Disemba kwa manispaa ya Geita pamoja na Halmashauri ya wilaya ya Geita huku akiwataka kutoa elimu ya ugonjwa wa Mabagi katika maeneo mbalimbali ya Maeneo hayo.
” Kwanza kabisa nitoe Maelekezo kwenye suala zima liusulo chanjo kama tulivyoambiwa hapa tunafahamu kabisa chanjo ni muhimu nielekeze kwamba elimu iendelee kutolewa kwa akina Mama , ” Katibu Tawala wilaya ya Geita, Lucy Beda.
Aidha Beda amewataka waratibu wa chanjo katika manispaa ya Geita pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kuhakikisha wanayafikia maeneo hatarishi ambayo yanakuwa na msongamano na watu kutoa elimu ili kujikinga na mlipuko wa magonjwa ya yasiyo ya kuambukiza .
“Huu ugonjwa wa Mabagi basi elimu iendelee kutolewa Mashuleni na wanafunzi waweze kuelewa vizuri lakini vile vile maeneo tofauti yenye msongamano wa watu tusiishie kuwapa elimu tuu maeneo yote ambayo ni hatarishi , ” Katibu Tawala wilaya ya Geita, Lucy Beda.
Afisa lishe kutoka Manispaa ya Geita , Pendo Makalangwa amesema kwa kila robo wamelenga kuwafikia jumla ya watoto 15782 kwa lengo la kutoa chanjo hasa katika maeneo ya manispaa ya Geita.