Afisa mmoja wa Umoja wa Mataifa katika mji wa Goma wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) unaokaliwa kwa mabavu, alisema jana Jumatano kuwa mji huo uko katika hali mbaya huku wasaidizi wa masuala ya kibinadamu wakipambana na hatari ya magonjwa ya mripuko.
Vivian van de Perre, Naibu Mwakilishi Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewaambia hayo waandishi wa habari kwa njia ya video na kusema: “Huku Goma, tunaendelea kuwa chini ya uvamizi; hali bado ni tete na hatari ya kuendelea vita na kuzuka magonjwa ya miripuko, inaongezeka.”
Amesema: “Waasi wa M23 na Jeshi la Rwanda (RDF) wanaendelea kuimarisha udhibiti wao ndani ya mji wa Goma na maeneo mengi ya jimbo la Kivu Kaskazini ambayo yalitekwa huko nyuma na waasi wa M23.”
“Njia zote za kutoka Goma ziko chini ya udhibiti wao, na uwanja wa ndege, pia uko chini ya udhibiti wa M23, na umefungwa,” ameendelea kusema van de Perre na kuongeza kuwa: “Ghasia zinazoongezeka zimesababisha mateso makubwa kwa binadamu, wamelazimika kuhama makazi yao na mgogoro wa kibinadamu nao umeongezeka.”
Van de Perre vile vile amesema kuwa, timu ya Umoja wa Mataifa huko DRC inayojulikana kwa jina la MONUSCO, pia inafanya kazi katika mazingira yenye changamoto nyingi. Maeneo yake muhimu katika kitovu cha ukanda huo yamezidiwa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na Wakongo waliokimbilia huko ili kunusuru maisha yao. Hii ni katika hali ambayo miundombinu ya timu hiyo ya Umoja wa Mataifa haikuundwa kwa ajili ya kutoa malazi makubwa na ya muda mrefu kwa wakimbizi.