Serikali ya Donald Trump imefichua nyaraka zinazoonyesha jinsi Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) lilivyofadhili miradi inayodaiwa kuwa isiyo na tija, huku baadhi ya fedha zikitolewa siku chache kabla ya matukio makubwa ya kisiasa na kijamii. Miongoni mwa matumizi hayo ni dola 500,000 kwa mradi wa kushughulikia ghasia za kimadhehebu Israel, siku 10 kabla ya shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023, na dola milioni 5 kwa EcoHealth Alliance, shirika lililohusishwa na utafiti wa virusi vya popo katika maabara ya Wuhan.
Nyaraka hizo pia zinaonyesha kuwa USAID ilitoa zaidi ya dola milioni 30 kwa miradi ya LGBT duniani, ikiwemo dola milioni 7.9 kwa waandishi wa Sri Lanka kujifunza lugha isiyoegemea jinsia, dola milioni 5.5 kwa uanaharakati wa LGBT Uganda, na mamilioni mengine kwa nchi kama Jamaica na Armenia. Aidha, kiasi cha dola milioni 10 za misaada ya chakula kinadaiwa kuishia kwa kundi lenye mafungamano na Al-Qaeda.
Miradi mingine ilihusisha dola milioni 25 kwa Deloitte kuendeleza usafiri wa kijani nchini Georgia, dola milioni 6 kubadili mitandao ya kidijitali kufuata misingi ya kidemokrasia ya kifeministi, na zaidi ya dola milioni 4.5 kwa kampeni dhidi ya habari potofu Kazakhstan. Serikali ya Trump ilisema hatua hii ni sehemu ya jitihada za kusimamisha matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.
Bilionea Elon Musk alijibu akitaja matumizi hayo kuwa “upotevu wa ajabu” wa pesa za wananchi. USAID, inayosimamia misaada ya maendeleo ya Marekani, ina bajeti ya kila mwaka ya makumi ya mabilioni ya dola, huku matumizi yake yakiidhinishwa na Bunge la Marekani.