Baada ya takribani miaka 12 kuzichezea timu mbili bora barani Ulaya na kusimama kwa muda huko Saudi Arabia, Neymar amerejea kucheza soka la kulipwa nchini kwao Brazil.
Nyota huyo wa zamani wa Barcelona na Paris Saint-Germain aliingia kama mchezaji wa akiba mwanzoni mwa kipindi cha pili kwa klabu yake ya utotoni ya Santos katika mechi yake ya Campeonato Paulista dhidi ya Botafogo SP Jumatano kwenye Uwanja wa Estádio Vila Belmiro.
Santos walikuwa wanaongoza mechi hiyo kwa bao 1-0 wakati Neymar alipoingia uwanjani lakini akakubali bao la kipindi cha pili, na mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1.
“Naipenda Santos. Sina maneno ya kuelezea nilichohisi usiku wa leo nilipokanyaga tena kwenye uwanja huu,” Neymar alisema baada ya mchezo huo.
Nyota huyo wa Brazil, ambaye alitajwa kuwa mchezaji bora wa mchezo huo, alikiri kwamba bado hajawa katika hali ya juu ya kimwili, lakini alisema alipata hisia chanya katika mechi yake ya kwanza katika kipindi cha miezi mitatu.
“Nahitaji dakika, kujiweka sawa michezoni. Siko kwa asilimia 100. Sikutarajia kukimbia na kupiga chenga nyingi sana usiku wa leo. Nadhani nitajisikia vizuri katika michezo minne au mitano,” aliongeza.
Neymar, ambaye alitimiza umri wa miaka 33 siku ya Jumatano, alikamilisha uhamisho wa kurejea Santos mnamo Januari 31, na kutia saini mkataba wa miezi sita ambao klabu hiyo ilisema inatumai kurefusha angalau Kombe la Dunia la 2026.
Alishinda mataji sita wakati alipokuwa Santos, iliyoko katika jiji la ufukweni nje ya São Paulo, likiwemo kombe la Copa Libertadores mwaka wa 2011.