Tume ya Ushindani Tanzania (FCC) imekutana na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu maboresho ya sheria na masuala mengine yanayohusu tume hiyo.
Akizungumza Februari 6,2025 wakati wa kikao kazi hicho, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, amesema vyombo vya habari ni mhimili muhimu unaotegemewa kufikisha taarifa kwa umma.
Amesema wanatumia kikao kazi hicho kuwajengea uwezo wahariri hao kuhusu Sheria ya Ushindani iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni ambayo tayari imepitishwa na Bunge na kusainiwa na Rais.
“Tunalishukuru sana Bunge letu na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kupitisha marekebisho ya Sheria ya Ushindani kwani itarahisisha ufanyaji biashara na uwekezaji nchini,” amesema Erio.
Wahariri hao pia wamejengewa uwezo kuhusu mienendo ya kibiashara inayokatazwa na sheria ya ushindani, tafiti, miungano ya makampuni na uraghbishi pamoja na udhibiti wa bidhaa bandia nchini.