Manchester City wamemjumuisha kiungo Rodri ambaye ni majeruhi katika kikosi chao kipya cha Ligi ya Mabingwa kwa awamu ya muondoano huku pia kuna nafasi kwa wachezaji wapya Omar Marmoush, Nico González na Abdukodir Khusanov.
Vitor Reis, ambaye pia aliwasili Januari kwa dili la €35 milioni ($36.2m) kutoka Palmeiras, ameachwa.
Marmoush, González na Khusanov wote watastahili kucheza mechi ya mchujo dhidi ya Real Madrid, itakayoanza wiki ijayo.
City, ambao walimaliza katika nafasi ya 22 kwenye jedwali la awamu ya ligi, watamenyana na wababe hao wa LaLiga katika mechi ya mkondo wa kwanza Uwanja wa Etihad siku ya Jumanne. Mechi ya mkondo wa pili itafanyika Bernabéu mnamo Februari 19.
Rodri atakosa michezo yote miwili huku akiendelea kupata nafuu kutokana na jeraha la goti alilolipata mwezi Septemba. Hata hivyo, kujumuishwa kwake kwenye kikosi cha Ligi ya Mabingwa kunaongeza uwezekano kwamba anaweza kucheza tena kabla ya msimu kumalizika.
Mshindi huyo wa Ballon d’Or amesema anatumai kurejea kwa wakati ili kushiriki Kombe la Dunia la Vilabu la FIFA, litakaloanza Marekani mwezi Juni.