Wanajeshi wapatao 75 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watapandishwa kizimbani leo, kwa kukimbia mapigano baada ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda kusonga mbele katika jimbo la mashariki la Kivu Kusini.
Taarifa iliyotolewa Jumapili na ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi ilisema kuwa askari hao pia wanashitakiwa kwa vurugu dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na mauaji na uporaji.
Wanajeshi 75 wanaokabiliwa na kesi walikamatwa kwa kukimbia mapigano baada ya kushikiliwa kwa mji wa Nyabibwe. Wanatuhumiwa kwa ubakaji, mauaji, uporaji na uasi, ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi imelieleza shirika la habari la Reuters.
Umoja wa Mataifa umeripoti ukiukaji mkubwa ikiwemo unyongaji, ubakaji wa magenge na utumwa wa kingono kufuatia msako mkubwa wa M23 mwishoni mwa mwezi Januari ambao ulipelekea kutekwa kwa mji mkubwa wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo