Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amelipongeza Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wazazi na Wananchi kwa kufanikisha Operesheni ya msako mkali na kuwapata Wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi Blessing Medium iliyopo Mwanza waliotekwa na kupatikana wakiwa salama.
Aidha, Bashungwa ametoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa amani na usalama na kueleza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vya Usalama limejipanga na lina uwezo na weledi wa kukomesha na kupambana na vitendo vyote vya kiuhalifu.
Bashungwa amesema hayo leo tarehe 11 Februari 2025 mkoani Mwanza mara baada ya kufika katika Shule ya Msingi Blessing Medium kuzungumza na Walimu na Wazazi pamoja na Askari na Maafisa waliofanikisha zoezi la kupatika kwa Wanafunzi waliotekwa tarehe 05/02/2025 na kupatikana tarehe 07/02/2025 wakiwa salama.
“Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, liko imara kitaaluma na lina vifaa vya kisasa na vingine havionekani na ndio maana linapokuja suala lolote linakuwa lipo imara, msifanye mchezo na weledi na utayari wa Jeshi la Polisi, mhalifu popote ulipo tuna uwezo wa kukufikia, tena bila kelele yoyote” amesema Bashungwa.
Kadhalika, Bashungwa ametoa wito kwa Wamiliki wa Shule kuanza utaratibu wa kufunga Kamera kwenye Mabasi na mazingira ya shule ili kuongeza ufuatiliaji na kuimarisha usalama wa wanafunzi kuanzia wanapotoka nyumbani hadi wanapokuwa katika mazingira ya shuleni.
Vile vile, Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camillus Wambura kupitia upya utaratibu wa kusajili kampuni binafsi za ulinzi pamoja kufuatilia mwenendo na weledi wao katika utendaji kazi.
Kwa Upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Muitafungwa amesema kuwa tukio la Utekaji wa Wanafunzi wawili lilitokea tarehe 05/02/2025 ambapo Jeshi la Polisi lilitimiza wajibu wake kwa kudhibiti uhalifu na kufanikiwa kuwapata Wanafunzi wakiwa salama.
Nae, mzazi wa mmoja wa Mwanafunzi, Anumie Mtweve ameishukuru Serikali kupitia Jeshi la Polisi kwa kuonesha ushirikiano mkubwa kwa wazazi na uongozi wa shule na kuhakikisha watoto wao wanapatikana wakiwa salama na bila shida yoyote.