Kijana mmoja ambaye bado hajafahamika Jina lake ameuwawa na wananchi wenye hasira kali katika Kijiji cha Nyakagwe Kata ya Nyankumbu mjini Geita, baada ya kukutwa na ng’ombe aliyeibwa kutoka kwa Mwananchi Mzee Dominic .
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo wananchi hao walimkamata kijana huyo alipokuwa akijaribu kutoroka na ng’ombe huyo na baada ya kuthibitisha kuwa mnyama huyo ni wa Mzee Dominic, walimshambulia hadi kufariki Dunia.
Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya wakazi wa maeneo hayo wamesema wizi wa mifugo umekuwa changamoto kubwa kwa zaidi ya miezi mitatu, hali iliyowafanya kuishi kwa hofu na wasiwasi.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kasemi Haruna Mozabiya, amesema kuwa katika eneo lao pekee tayari zaidi ya ng’ombe 12 wameibwa kati ya Novemba mwaka Jana na Januari mwaka huu huku akiiomba serikali kuingilia kati tatizo hilo licha ya tukio hilo la wananchi kujichukulia sheria mkononi ili kuimarisha usalama wa mifugo na kupunguza mateso kwa wafugaji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita SACP. Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa tukio na kusema tukio hilo limetokea February 8 mwaka huu katika kijiji cha Nyakagwe kata ya Nyankumbu ambapo mwananchi mmoja aliibiwa ng’ombe zake wawili na kufanikiwa kupiga kelele ndipo wananchi wenye hasira kali walimshushia kipigo mwizi huyo na kufariki Dunia.