WAFUNGWA WALIOMALIZA VIFUNGO VYAO WATUHUMIWA KWA WIZI WA MIFUGO GEITA.
Jeshi la Polisi Mkoani Geita limesema litaendelea kukabiliana na changamoto ya wimbi la wizi wa mifugo katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo ambapo Jeshi la Polisi limesema wizi huo unachangiwa na Baadhi ya wafungwa ambao wamekamilisha vifungo vyao Gerezani na kurudi uraiani.
Hayo yameelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita , SACP Safia Jongo wakati akitolea ufafanuzi wa uwepo wa wimbi la wizi wa Mifugo ambalo limeendelea kukithiri katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo huku akisema tayari wamejipanga kufanya Oparesheni kukabiliana na wimbi hilo.
” Ni kweli tulikuwa na wimbi kubwa la wizi wa mifugo Mkoa wa Geita tulipambana na asilimia kubwa watuhumiwa walikamatwa na kufikishwa mahakamani na chanzo cha Matukio haya kurudi kwanza watuhumiwa walifungwa kwa muda mchache wengine Miezi sita wengine mwaka ambapo baada ya kutumikia vifungo vyao wamerudi na kuanza kufanya upya uharifu huo , ” Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita SACP. Safia Jongo.
” Sisi kama Jeshi la Polisi mikakati tuliyonayo moja wapo ni hiyo kuwasisitiza wananchi kujenga Mazizi salama lakini kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi hasa sungusungu ili wao na Sisi tushirikiane kuendelea tena kupambana na hawa watuhumiwa lakini pia oparesheni mbalimbali zimepangwa ikiwemo kukagua mabucha bubu kwa sababu haya mabucha bubu nayo yanachangia kuuza hizo nyama ambazo zinaibiwa , ” Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, ” SACP. Safia Jongo.