Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) siku ya Jumatatu limelaani uporaji wa maghala yake mwishoni mwa wiki hii iliyopita huko Bukavu, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusini, huku kukiwa na sintofahamu juu ya hali ya usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Maghala muhimu ya chakula kilichohifadhiwa yalikusudiwa kutoa msaada wa kuokoa maisha kwa familia zilizo hatarini zaidi ambazo sasa zinakabiliwa na janga la kibinadamu linalokua,” shirika hilo la Umoja wa Mataifa limesema kwenyemtandao wa kijamii wa X.
WFP imebainisha kuwa wakati unyanyasaji unapoenea, upatikanaji wa chakula unazidi kuwa mgumu, ikiongeza kuwa iko tayari kuanza tena usaidizi muhimu wa chakula kwa walio hatarini zaidi mara tu kutakapokuwa salama kufanya hivyo.
“Tunatoa wito kwa haraka kwa pande zote kwenye mzozo kuheshimu majukumu yao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na ulinzi wa raia na wafanyakazi wa kibinadamu,” WFP imesema.
Tukio hilo lilikuja baada ya waasi wa M23 wanaopigana na vikosi vya Kongo kudai siku ya Ijumaa ya wiki iliyopita kuteka uwanja wa ndege wa Kavumu, ulioko kilomita 25 kutoka mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kusii, Bukavu, mashariki mwa DRC.
Waasi wa M23 waliingia pia Bukavu, baada ya kuteka Kavumu.
Siku ya Jumapili Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilisema kwamba jeshi la Rwanda na washirika wake wameingia katika mji wa Bukavu na kuwataka wakazi kuendelea kuwa macho.