Tanzania Mortgage Refinance Company Limited (TMRC) leo imeikaribisha Benki ya KCB Tanzania Limited kama mwanahisa wake mpya. Benki ya KCB Tanzania Limited imejiunga na TMRC kama mbia wa 20 kufuatia uwekezaji wa mtaji wa TZS 500 milioni katika TMRC.
Uwekezaji huu wa Benki ya KCB katika TMRC ulihitimishwa Desemba 2024. KCB Bank inaungana na wanahisa wengine wa TMRC wa taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na CRDB Bank Plc; Benki ya NMB Plc; Benki ya Taifa ya Biashara (NBC); TIB Development Ltd; Azania Bank Plc; Exim Bank (T) Ltd na DCB Commercial Bank Plc. Wanahisa wengine wa TMRC wa taasisi za fedha ni pamoja na Access Bank Ltd; Benki ya Afrika (T) Ltd (BOA); First Housing Finance Ltd; Peoples Bank of Zanzibar Ltd (PBZ); I&M Bank (T) Ltd; NCBA Bank Ltd , Mkombozi Commercial Bank Plc na Mwanga Hakika Bank(MHB).
Umiliki wa hisa wa TMRC unajumuisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Taasisi za Fedha za Maendeleo ya Kimataifa (DFIs) kama vile Shelter Afrique (taasisi ya kifedha ya Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) ambalo ni sehemu ya Kundi la Benki ya Dunia.
Kwa hatua ya Benki ya KCB kujiunga na TMRC, inamaanisha benki hiyo itaweza kupata fedha nyingi zaidi kwa madhumuni ya mikopo ya nyumba kutoka TMRC kama sehemu ya mkakati wake wa kukuza biashara yake kupitia utoaji wa mikopo ya nyumba.
Akizungumza wakati wa mkutano na wanahabari, Mkurugenzi wa Biashara wa Kanda wa KCB Group na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania, Bw. Cosmas Kimario, alisema hatua hiyo itaongeza tija katika kuimarisha ukwasi ili kupanua wigo wa huduma za mikopo ya nyumba inayotolewa na benki hiyo hapa nchini.
“Kwa miaka mingi, KCB Bank Tanzania imekuwa mshirika wa kuaminika katika sekta ya mikopo ya nyumba, ikitoa suluhisho bunifu za kifedha zinazowawezesha watanzania wengi kumiliki makazi yao. Kupitia uwekezaji huu, tunajizatiti zaidi katika kusaidia maendeleo ya sekta ya nyumba kwa kuleta suluhisho endelevu na kuongeza fursa za ujenzi wa nyumba nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa, kwa kujiunga na kuwa mwanahisa wa TMRC, inamaanisha kikomo cha ufadhili wa fedha wa muda mrefu kwa benki hiyo kutoka TMRC kitaongeza hadi Sh10 bilioni ikiwa ni mara ishirini ya uwekezaji huo.
“Hii inamaanisha kwamba benki ya KCB itapata kuwa na fedha zaidi ambazo zitaelekezwa kwenye mikopo ya nyumba kwa wateja wetu ili kukidhi mahitaji ya soko ya sasa ya mikopo ya nyumba na kutatua changamoto ya uhaba wa nyumba za makazi unaokabili taifa letu,” alisema.
Kufikia Septemba 2024, KCB Bank ilishika nafasi ya nane (8) katika sekta ya benki kwa mujibu wa ripoti ya BOT, ikitoa mikopo yenye thamani ya TZS 34.1 bilioni na kushikilia sehemu ya soko ya (market share) 4.75%, huku wateja 175 wakinufaika na mikopo hiyo.