Idara ya Taifa ya Polisi nchini Japani inasema imewatambua raia 11 wa Nigeria ambao wanashukiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutoka kwa raia wa Japani kwa njia ya kimapenzi na utapeli mwingine.
Maafisa wa idara hiyo wanasema walifuatilia fedha zilizopatikana kwa njia ya udanganyifu katika mapenzi na uwekezaji uliofanyika kuanzia mwaka 2022 hadi 2023 ukilenga watu nchini Japani. Maafisa hao wanasema wamekuwa wakifanya uchunguzi wa pamoja wa kundi hilo na mamlaka za Nigeria.
Wanachama wa kundi lenye makazi yake nchini Nigeria wanatuhumiwa kutuma jumbe za moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii, wakitumia utambulisho wa uongo kama vile daktari na mwanaanga.
Wanatuhumiwa kuwatapeli watu 14 wa Japani jumla ya yeni milioni 150 ama takribani dola za Kimarekani 990,000 kwa kisingizio cha gharama za ndoa na uwekezaji.
Maafisa wa idara hiyo ya polisi pia wanasema wamewatambua raia tisa wa Japani ambao wanashukiwa kuzibadilisha fedha zilizotapeliwa kuzifanya mali za kificho na kupokea fidia kutoka kwa kundi hilo lenye makazi nchini Nigeria.
Hasara ya utapeli wa uwekezaji na kimapenzi kwa kutumia mitandao ya kijamii ilikuwa ni jumla ya yeni bilioni 126.8 ama takribani dola za Kimarekani milioni 830 mwaka 2024 nchini Japani.