Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amewahimiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kushirikiana na Viongozi wa Serikali za Mitaa katika Manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha udhibiti wa upotevu wa maji mitaani pamoja na kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya maji.
Ameeleza hayo wakati wa kikao kazi cha Mamlaka na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kilichoitishwa na DAWASA na kusisitiza kuwa hatua hii itasaidia kuleta ufanisi katika shughuli zinazotekelezwa na Mamlaka za kuboresha huduma.
Ameeleza kuwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ndio daraja muhimu la kuwafikia wananchi wengi kwenye makazi yao ili kuweza kudhibiti upotevu wa maji sambamba na kuwashirikisha wananchi kwenye jitihada za kulinda miundombinu ya maji.
Ameongeza kuwa, Viongozi wanapaswa kupewa taarifa za kila hatua inayochukuliwa ikiwemo panapotokea hitilafu ya uzalishaji na usambazaji wa maji kwenye Mtambo au kwenye mifumo ya maji.
“Hitilafu zinapotokea, Viongozi wapewe taarifa na washirikishwe ili wajue namna ya kuwasiliana na wananchi kwa lengo la kuondoa sintofahamu,” amesema Mhe. Aweso.
Pia ameitaka DAWASA kutekeleza zoezi la kuhamasisha wananchi kuwa na utaratibu wa kutunza na kulinda maji kwenye vyombo vikubwa, ili kuepuka usumbufu pale panapotokea hitilafu.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Sadi Mtambule ameipongeza DAWASA kwa jitihada hizi za kuwashirikisha Viongozi wa Serikali za Mitaa katika kazi mbalimbali zinazotekelezwa za utoaji wa huduma.
“Tunashukuru kwa jitihada hizi za zinazosaidia kuchochea ulinzi wa miundombinu ya maji, pamoja na kudhibiti upotevu wa maji kwenye maeneo ya makazi ya wananchi,” ameeleza Mhe Mtambule.
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Waziri Aweso alivyoagiza ya kuwashirikisha Viongozi wa Serikali za Mitaa ili kurahisisha ufuatiliaji wa huduma mitaani pamoja na kudhibiti upotevu wa maji kwenye maeneo ya wakazi.