Rwanda imesitisha ushirikiano wake wa kutoa misaada na Ubelgiji, kufuatia ukosoaji wa Brussels wa kuhusika kwa Kigali katika mzozo unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Ubelgiji inaishutumu Rwanda kwa kuhujumu utimilifu wa ardhi ya DRC kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, ambao wameteka miji miwili mikubwa mashariki mwa nchi hiyo katika wiki za hivi karibuni.
Ikikasirishwa na ujumbe huu, Rwanda ilitangaza Jumanne kwamba inasitisha mpango wake wa msaada wa nchi mbili wa 2024-2029 na Ubelgiji.
Mamlaka ya Rwanda ilitoa taarifa Jumanne ikidai kuwa Brussels inahujumu upatikanaji wake wa “fedha za maendeleo, zikiwemo taasisi za kimataifa”.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Rwanda iliongeza kuwa Ubelgiji ina haki ya kuchagua upande katika mzozo wa DRC lakini inapaswa kuacha “kuingiza siasa kwenye maendeleo”.
Naibu Waziri Mkuu wa Ubelgiji Maxime Prévot alisema kwenye X kwamba serikali ya Ubelgiji imetambua uamuzi wa Rwanda.
“Tumejitolea kwa mchakato wa kusimamishwa kitaaluma ambao utahifadhi mafanikio ya ushirikiano wetu wa muda mrefu kwa manufaa ya watu wa Rwanda,” aliandika.
“Tumedhamiria kuendeleza juhudi zetu za kuongeza ufahamu na kuhamasisha jumuiya ya kimataifa kutafuta suluhu la amani la mzozo wa mashariki mwa DRC, kwa kuzingatia sheria za kimataifa,” aliongeza.
Mapigano mashariki mwa DRC ni sehemu ya mzozo wa miongo kadhaa ambao una mizizi katika mvutano wa kikabila.