Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kwa kushirikiana na Shirika la Utangazaji la Tanzania (TBC), wameendesha zoezi la upandaji miti katika Shule ya msingi Kapeta, lengo likiwa ni kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na kutunza mazingira ya karibu na mgodi wa STAMICO.
Zoezi hilo liliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayoub Rioba Chacha, kama sehemu ya juhudi za kuhakikisha kwamba mradi wa STAMICO licha ya uzalishaji wa nishati safi kupitia makaa ya mawe, pia unachangia katika utunzaji wa mazingira.
Dkt. Rioba alisema kwamba juhudi za upandaji miti ni muhimu kwa ajili ya kulinda mazingira na kuongeza mchango wa Shirika katika ustawi wa jamii na maendeleo endelevu.
Alisisitiza kuwa TBC itaendelea kushirikiana na STAMICO katika miradi ya mazingira na maendeleo, hasa katika maeneo yanayozunguka migodi.
Naye, Mkuu wa Masoko na Uhusiano kutoka STAMICO Bw. Gabriel Nderumaki amesema katika zoezi hilo, ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya 6 Katika kutunza mazingira na kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia ya RafikiBriquettes.
Akizungumza katika zoezi hilo, Anitha Jonathan, Afisa Elimu na Mahusiano Mwandamizi kutoka Ofisi ya Hati Miliki Tanzania, alitoa pongezi kwa TBC na STAMICO kwa kuonyesha umuhimu wa utunzaji wa mazingira. Alisema, “Kupanda miti ni hatua muhimu ya kuhifadhi mazingira na kutoa alama ya kijani ambayo itachangia katika juhudi za kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo.”
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Kapeta Sayuni Ayubu, alielezea furaha yake kutokana na hatua ya TBC na STAMICO kupanda miti katika shule hiyo. Aliahidi kushirikiana na wakazi wa eneo hilo katika kuhakikisha miti hiyo inalindwa na kutunzwa kwa faida ya jamii, na kuongeza kuwa hii ni fursa muhimu ya kuboresha mazingira na kutoa mchango wa kudumu kwa maendeleo ya kijamii.
Zoezi hili linajumuisha juhudi za shirika la STAMICO na TBC katika kuhakikisha mazingira ya mgodi na maeneo jirani yanahifadhiwa, ili kuwa na mazingira bora kwa ustawi wa jamii na kizazi kijacho.