Mshambulizi wa zamani wa klabu ya Manchester City na timu ya taifa ya Argentina Sergio Kun Aguero alipoteza dau lingine Jumapili kufuatia vijana wa Pep Guardiola kuchapwa na Liverpool.
Aguero alikuwa ameonyesha matumaini yake makubwa kwa klabu yake ya zamani kushinda katika mechi hiyo kubwa iliyochezwa katika uwanja wa Etihad kwa kuwekelea dau kubwa.
Muargentina huyo mwenye umri wa miaka 36 alikuwa ameweka dola 5,000 (Sh647,250) kwa Man City kushinda ambapo angepata $11,300 (Sh 1.46m) kama malipo.
Man City hata hivyo walipokea kichapo katika uwanja wao wa nyumbani huku The Reds wakiondoka na ushindi wa 0-2, kumaanisha dau la Aguero liliungua.
Hii ni mara ya pili imani ya Muargentina huyo kwa klabu yake ya zamani inamletea shida katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Takriban wiki mbili zilizopita, Aguero alijikuta katika hali ya utata baada ya ahadi yake tata kabla ya mechi ya Ligi ya Mabingwa kati ya Manchester City na Real Madrid.
Kabla ya mchuano huo uliofanyika kwenye uga wa Etihad, Agüero alitoa kauli yenye utata akisema, “Ikiwa Real Madrid itashinda, nitakata tezi ndume zangu.”
Maneno haya, ambayo yalionekana kama mzaha wa kuonesha imani yake kwa City, sasa yamegeuka mzigo mzito baada ya Real Madrid kuibuka na ushindi wa 2-3.