Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama cha Mapinduzi UVCCM Mkoa wa Geita wamewataka vijana kuchangamkia Fursa za Mikopo ya Asilimia 10 katika Halmashauri zote za Mkoa huo na kuachana na vitendo vya wizi wa Mifugo ambavyo vimekuwa vikiripotiwa katika vyombo mbalimbali.
Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana ya Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita , Manjale Magambo wakati alipotembelea na kukagua uhai wa chama cha Mapinduzi , Kushiriki katika fursa za Mikopo pamoja na kuhamasisha vijana kushiriki katika uchaguzi Mkuu katika kata mbalimbali ikiwemo kata ya kasamwa.
“Ndugu zangu tumekuja kukemea mambo haya serikali ya CCM haiungi Mkono wizi wa Mifugo tunahitaji vijana wafanye kazi na ndio maan Dkt. Samia Suluhu Hassan amerejesha mikopo hii ikiwa imeboreshwa vijana wenzangu mambo ya wizi yameshapitwa na wakati tuchangamkieni Fursa , ” Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Geita, Manjale Magambo.
Aidha Manjale amesema ni vyema vijana wakawa na mchango mkubwa katika kulisaidia Jeshi la Polisi kutokana na idadi yao kuwa ndogo katika kukomesha vitendo hivyo huku akiwataka kuunda vikundi kwa ajili ya kuchukua mikopo hiyo ambayo kwa sasa inatolewa na Halmashauri kote nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Geita Bi. Naomi Fujo amewataka vijana kuwa mstari wa mbele katika kuthamini amani tuliyo nayo ambapo amewahasa vijana kuwa wazalendo na kuwa mstari wa mbele kushiriki katika Uchaguzi mkuu wa 2025.
\