Tume ya Kudhibiti UKIMWI Uganda (UAC) imetoa wito kwa Bunge na Wizara ya Fedha kufanya mabadiliko katika vipaumbele vya bajeti ya nchi hiyo na kutenga zaidi ya dola milioni 81.3 (Shilingi bilioni 300) za ziada ili kukabiliana na pengo la ufadhili lililoachwa na uamuzi wa serikali ya Marekani kusitisha misaada kutoka nje.
Hii inafuatia amri ya utendaji iliyotiwa saini na Rais wa Marekani Donald Trump kusitisha misaada kwa baadhi ya miradi.
Wito huo ulitolewa na Dkt. Vincent Bagambe, Mkurugenzi wa Mipango na Mikakati katika UAC, ambaye alifika mbele ya Kamati ya Afya ya Bunge mnamo Februari 11, 2025.
Katika taarifa yake mbele ya kamati, alisisitiza haja ya dharura ya kuongezeka kwa mgao wa bajeti, haswa kwa bidhaa muhimu.
“Tunalishauri bunge kuangalia upya vipaumbele vya bajeti na kuongeza fedha kwa ajili ya huduma za kudhibiti ukimwi kwa kuongeza zaidi ya dola milioni 81.3 (Shilingi bilioni 300) ili kugharamia dawa, vifaa vya maabara na rasilimali nyingine zilizotolewa na PEPFAR,” Bagambe alisema.