Mahakama ya Tunisia Jumanne iliwahukumu kifo washtakiwa nane kwa tuhuma za kumuua Mohamed Brahmi, kiongozi wa upinzani wa mrengo wa kushoto mwaka 2013.
Shirika la habari la serikali ya Tunisia limenukuu taarifa ya msemaji wa mahakama ikisema kuwa washtakiwa watatu pia walipata hukumu za ziada za kifo kwa kile alichosema ni “kushiriki kimakusudi katika mauaji ya kukusudia.”
Mashtaka dhidi yao pia yalijumuisha “kujaribu kubadilisha asili ya serikali” na “kuchochea mauaji na migogoro ya silaha.”
Mfungwa wa tisa, ambaye yuko mbioni, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela, “kwa kushindwa kuripoti kwa mamlaka alichokuwa nacho kuhusu uhalifu wa kigaidi,” shirika la utangazaji la Tunisia liliongeza.
Mnamo Julai 25, 2013, mwanasiasa Mohamed Brahmi, kiongozi wa Movement of the People Party, alipigwa risasi nje ya nyumba yake.
Mauaji yake wakati huo yalizua mzozo wa kisiasa nchini humo.