Waendesha mashtaka nchini Mauritania wameiomba mahakama ya rufaa kumhukumu rais wa zamani Mohamed Ould Abdel Aziz kifungo cha miaka 20 jela kwa matumizi mabaya ya ofisi.
Aziz kwa sasa anakata rufaa ya kifungo cha miaka mitano alichopata mwaka 2023 baada ya kukutwa na hatia ya kutumia nafasi yake kujilimbikizia mali akiwa madarakani kuanzia 2008 hadi 2019.
Waendesha mashtaka wanataka mahakama ya rufaa badala yake iongeze kifungo cha awali cha kifungo.
Mwendesha mashtaka mkuu, Sidi Mohamed Ould Di Ould Moulay, aliiambia mahakama mjini Nouakchott kwamba kiongozi huyo wa zamani “alibadilisha urais kuwa ofisi … kwa ajili ya kuwahadaa wawekezaji”.
Aziz anaaminika kujilimbikizia mali na mtaji wenye thamani ya dola milioni 70 wakati wa urais wake.
Mwendesha mashtaka pia aliiomba mahakama kufuta shirika la hisani la Rahma, shirika ambalo alisema lilianzishwa na mtoto wa Aziz kwa malengo haramu.
Rais huyo wa zamani ambaye amekuwa kizuizini tangu kesi yake ya awali ilipoanza Januari 2023, alikuwa akihudhuria pamoja na maafisa wakuu na washauri kadhaa wa zamani.
Pia wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi, kujitajirisha haramu, biashara ya ushawishi na utakatishaji fedha.
Aziz anakanusha mashtaka dhidi yake.