9Watu 11 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa Alhamisi wakati wa mlipuko katika mji wa mashariki mwa Congo wa Bukavu uliotokea kwenye mkutano wa hadhara ulioongozwa na viongozi wa kundi la M23, ambalo lilichukua udhibiti wa mji huo mapema mwezi huu.
Viongozi wa waasi wameituhumu serikali ya Congo kwa shambulizi hilo la bomu na kusema washambuliaji ni miongoni mwa waliouawa katika mlipuko huo, huku kukiwa ripoti za kukinzana kati ya waasi na maafisa wa eneo hilo kuhusu idadi ya washambuliaji na waathirika.
Rais wa Congo ameyatuhumu “majeshi ya kigeni” ambayo hakuyataja kuhusika na shambulizi hilo.
“Shambulizi hilo lilisababisha vifo vya watu 11 na uchunguzi unaendelea. Muhusika wa shambulizi hilo ni miongoni mwa waathirika,” Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa Congo River Alliance (AFC), ambao unajumuisha M23, aliwambia waandishi wa habari.
“Kuna watu 65 waliojeruhiwa, sita kati yao wako katika hali mbaya na wanapewa matibabu katika chumba cha upasuaji.”
Viongozi wa M23, akiwemo Nangaa walikuwa wanakutana na wakazi wakati mlipuko huo ulipotokea mjini kati Bukavu.
M23 imeitumu serikali ya Congo kwa kupanga shambulizi hilo.