Bahati Nasibu ya Taifa Tanzania imetangaza ushirikiano wa kimkakati na Mixx by Yas. Hii ikiwa ni hatua muhimu inayolenga kuimarisha uwepo wake sokoni kuelekea kwenye kilele cha uzinduzi rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa unaosubiriwa kwa hamu kubwa.
Ushirikiano huu na Mixx by Yas unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha wateja wanaotumia mtandao wa Yas wanapata fursa ya kununua tiketi kiurahisi mara tu baada ya uzinduzi rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa hivi karibuni.
Kupitia wateja wake zaidi ya milioni 23, Yas Tanzania itahakikisha ununuzi wa tiketi unakuwa rahisi kwa kutumia mifumo yake ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na huduma za fedha kwa njia ya simu, USSD codes, na Super App ya Mixx by Yas.
Aidha, wateja wanaotumia Mixx by Yas watanufaika na taarifa za hapo kwa papo, promosheni, na maudhui maalum yanayohusiana na Bahati Nasibu ya Taifa. Ushirikiano huu pia utarahisisha safari ya mteja kwa kuwawezesha kununua tiketi na kudai ushindi kupitia mifumo waliyoizoea na kuiamini, hivyo kuongeza urahisi na upatikanaji wa huduma kote nchini.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Bw. Kelvin Koka, Mkurugenzi wa ITHUBA Tanzania—mwendeshaji rasmi wa Bahati Nasibu ya Taifa kwa kipindi cha miaka minane—amesisitiza umuhimu wa kushirikiana na chapa zenye sifa kubwa kwa mafanikio ya uzinduzi:
“Bahati Nasibu ya Taifa Tanzania imeundwa kama rasilimali ya kitaifa inayolenga kutoa thamani, burudani, na manufaa ya kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania. Ushirikiano wetu na Mixx by Yas ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kushirikiana na taasisi zinazoheshimika na kushiriki maono yetu. Pamoja, tutatengeneza fursa shirikishi na rahisi kupitia jukwaa la Bahati Nasibu kwa Watanzania wote.”
Kwa upande wake Bi. Angelica Pesha, Afisa Mkuu wa Mixx by Yas, alielezea furaha yake kuhusu ushirikiano huu:
“Tuna furaha kubwa kuwa sehemu ya mpango huu wa mabadiliko. Bahati Nasibu ya Taifa Tanzania ni fursa adhimu ya kuwahusisha Watanzania kwa njia bunifu. Kwa kutumia mifumo yetu ya kidijitali na suluhisho za kifedha, tutahakikisha wateja wetu wanapata huduma za Bahati Nasibu ya Taifa Tanzania kwa njia rahisi na salama. Sisi kama sehemu ya Mixx by Yas, tunaamini katika kushirikiana na miradi inayochochea ukuaji na ubunifu, na tunatazamia kuchangia mafanikio ya uzinduzi huu Bahati Nasibu ambao tunaamini utakuwa ni wa kihistoria.”
Ushirikiano huu kati ya Bahati Nasibu ya Taifa Tanzania na Mixx by Yas unatarajiwa kubadilisha jinsi Watanzania wanavyoshiriki katika shughuli za bahati nasibu. Kwa kuchanganya miundombinu thabiti ya kidijitali ya Yas Tanzania na mikakati madhubuti ya ushiriki wa wateja, pamoja na mvuto mkubwa wa Bahati Nasibu ya Taifa Tanzania, ushirikiano huu utawezesha upatikanaji wa huduma za Bahati Nasibu ya Taifa hasa katika maeneo ya mijini na pembezoni mwa miji.
Kupitia ujumuishaji wa huduma za Bahati Nasibu kupitia Super App ya Mixx by Yas, kununua tiketi na kupata maudhui yanayohusiana na Bahati Nasibu kutakuwa rahisi zaidi kwa mamilioni ya Watanzania. Hatua hii ya kimkakati inatarajiwa kuimarisha juhudi za kufikia watu wengi, kuongeza hamasa kwa umma, na kuhakikisha ushiriki mpana wa makundi mbalimbali ya watu.
Kadri maandalizi ya uzinduzi rasmi yanavyoendelea, ushirikiano huu unalenga kuweka kiwango kipya cha ushirikiano wa kidijitali katika tasnia ya Bahati Nasibu ya Taifa.