Michuano ya kombe la Kagame linaloendelea nchini Rwanda imeendelea kushika kasi.
Leo hii klabu bingwa ya Tanzania Azam FC ilijitupa dimbani kwa mara 3 kwa kucheza dhidi ya Atlabara ya Sudan Kusini.
Matokeo ya mchezo huo ni sare ya 2-2, huku mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC, mburundi Didier Kavumbagu akiinusuru Azam kupata kipigo baada ya kuisawazishia Azam dakika ya 86, baada ya krosi ya Shomary Kapombe.
Azam ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na kiungo Kipre Michael Balou kwa shuti la mpira wa adhabu kutoka umbali wa mita 20, baada ya pacha wake, Kipre Herman Tchetche kuangushwa.
Atlabara ilirudi vizuri kipindi cha pili na kufanikiwa kusawazisha bao dakika ya 48, mfungaji Nahodha wake, Thomas Batista kabla ya kufunga la pili dakika ya 60 mfungaji Bony Martin.
Atlabara ilipata pigo dakika ya 89 baada ya Nahodha wake, Batista kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Shomary Kapombe akiruka kwenda chini baada ya kuchezewa rafu na beki wa Atlabara
Kwa matokeo hayo, Azam inafikisha pointi tano baada ya mechi tatu na kujihakikishia nafasi ya kwenda Robo Fainali ya michuano hiyo, wakati Atlabara inafikisha pointi mbili baada ya mechi mbili.