Serikali ya Nigeria imesema wamefikia makubaliano ya kusitisha mapambano na kikundi cha wapiganaji wa Boko Haram, ambapo katika taarifa rasmi iliyotolewa kuhusiana na makubaliano hayo imesema kuwa wameafikiana kuhusu kuachiliwa huru kwa wasichana zaidi ya 200 waliotekwa nyara huko Chibok.
Kwa mujibu wa katibu mkuu wa serikali ya Nigeria, Hassan Tukur amesema maafikiano hayo yamefikiwa leo baada ya kumalizika kwa mazungumzo baina ya upande wa serikali na wawakilishi wa kikundi hicho, yaliyodumu kwa takribani mwezi mmoja.
Serikali imesema imekuwa ikifanya mazungumzo na viongozi wa Boko Haram mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na yale yaliyofanywa mara mbili nchini Chad chini ya uongozi wa Rais wa Chad, Idris Derby.
Tukur amesema kuwa Boko Haram wamekubali kuwaachilia huru wasichana waliotekwa nyara mjini Chibok, japo muafaka zaidi juu ya hilo utapatikana punde baada ya kumalizika mkutano mwingine unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini Chad.
Bado haijafahamika kama makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili yanahusisha na matakwa yaliyotolewa awali na kundi la Boko Haram kutaka kubadilishana wasichana hao na wafungwa ambao ni wapiganaji wa kikundi hicho wanaoshikiliwa na serikali ya Nigeria.