Uhaba mkubwa wa dawa na vifaa vya tiba umezikumba hospitali nyingi nchini zikiwemo Muhimbili na Ocean Road kutokana na Serikali kudaiwa zaidi ya bilioni90 na Bohari kuu ya dawa nchini MSD.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la SIKIKA Irene Kiwia alisema hali hiyo inahatarisha maisha ya wananchi kutokana na kukosa matibabu kwani Bohari hiyo inaidai Serikali fedha nyingi.
Kiwia alisema kutokana na madeni hayo MSD imesitisha usambazaji wa dawa katika hospitali za Serikali ambazo zinadaiwa mamilioni ya shilingi huku akitolea mfano hospitali ya Muhimbili inadaiwa bilioni nane.
Kwa mujibu wa Kiwia alisema ongezeko la deni hilo limekua linaathiri utendaji kazi wa MSD kwa kuwa taasisi hiyo haijiendeshi kwa faida.
NIPASHE
Historia mpya imeandikwa Tanzania na vyama vinne vya siasa baada ya kutiliana saini makubaliano ya ushirikiano katika kusaka katiba mpya na kushirikiana kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani katika nafasi zote.
Vyama hivyo jana vilitiliana saini makubaliano hayo hadharani katika mkutano mkuu wa hadhara uliofanyika viwanja vya Jangwani Dar s salaam ukiratibiwa na Ukawa.
Vyama hivyo ni Chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA,Chama cha wananchi CUF,NCCR-Mageuzi na NLD huku majina ya waliosaini ni Ibrahimu Lipumba,Maalim Seif,Freeman Mbowe,Wilbroad Slaa,James Mbatia na Mosena Nyambabe.
Makubaliano hayo ni pamoja na kuhusisha sera za vyama,kusimamisha wagombea wa pamoja kwenye ngazi zote,namna ya vyama hivyo vitakavyoshirikiana katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na ule uchaguzi mkuu mwakani.
MWANANCHI
Mzee wa miaka62 Rashid Mbogo amepandishwa kizimbani katika mahakama ya Wilaya ya Mpanda kwa tuhuma za kumbaka mjukuu wake mwenye miaka mitano.
Ilidaiwa na mwendesha mashtaka Chiganga Ntengwa kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo usiku akiwa nyumbani kwake ambapo alimwita mjukuu wake huyo na kumpakata mapajani kisha kumvua nguo zote na kuanza kumbaka.
Alisema kuwa baada ya mkewe aliyekua akiandaa chakula jikoni kusikia kelele za mjukuu wake alitoka mbio pamoja na majirani na walipofika ndani walikuta mjukuu wake akitokwa damu nyingi sehemu za siri.
Mshtakiwa alikana kosa hilo lakini alishindwa kutoka kwa dhamana baada ya kushindwa kukamilisha dhamana na kuwekwa rumande.
MWANANCHI
Uongozi wa Klabu ya Simba umewatimua kambini nyota wake watatu Shaban Kisiga,Haruna Chanongo na Amri Kiemba bada ya wachezaji hao kucheza chini ya kiwango katika mechi za ligi kuu Tanzania bara.
Uamuzi huo wa kuwatimua kambini ulipatikana baada ya kikao cha kamati ya utendaji ya Simba kukutana jana Mkoani Mbeya mara baada ya mchezo wao dhidi ya Prison walioendeleza sare kwa kutoka 1-1.
Chanzo cha habari ndani ya kamati hiyo kilisema benchi la ufundi limepewa mechi tatu nz wakishindwa kufanya vizuri yatafanyika mabadiliko kwani mwenendo wa timu ni mbaya sana.
MTANZANIA
Vita ya urais inazidi kupamba moto baada ya Waziri wa nchi ofisi ya Waziri mkuu Profesa Mark Mwandosya kutangaza rasmi kuwania nafasi hiyo uchaguzi ujao.
Mwandosya ameweka wazi mikakati yake kuelekea katika mchakato huo akisema yupo tayari kuwatumikia wananchi kwa uadilifu ingawa yeye ni maskini na hana fedha za kuwanunua wajumbe wampigie kura.
Pamoja na mambo mengine alisema anashangazwa na baadhi ya watu ambao wamekua wakitumia fedha kutafuta nafasi mbalimbali za uongozi na alihoji fedha hizo wanazitoa wapi na kwa maslahi ya nani.
MTANZANIA
Wanafunzi592 wameacha masomo na kuolewa huku wengine371 wakibainika kuwa na ujauzito katika shule mbalimbali za Unguja na Pemba.
Mbali na hao wanafunzi62 wamebainika kuambukizwa vurusi vya Ukimwi kati ya wanafunzi7770 waliopimwa kwa mwaka2005-2013.
Takwimu hizo zilitolewa na Katibu Umoja wa Serikali ya wanafunzi Salum Humud wakati wa sherehe za kutimiza miaka mitano ya kuasisiwa kwa umoja huo na kusema kuna tatizo kubwa la kutokuwepo na ushirikiano baina ya walimu na wazazi.
Naibu Waziri wa Habari,Utamaduni na Utalii Hindu Hamad alisema alisikitishwa na hali hiyo huku akiwataka wazazi,walimu kushirikiana katika kutoa taarifa za maendeleo ya masomo kwa wanafunzi.
MTANZANIA
Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji MOI imeendelea kuwa nguzo muhimu nchini kwa utoaji wa huduma za tiba za upasuaji.
Ofisa uhusiano Moi Patrick Mvungi alisema MOI imesaidia kuokoa asilimia95 ya Watanzania ambao kwa namna moja ama nyingine wangeweza kupoteza maisha yao ama kupata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali.
Aliongea pia zaidi ya asilimia99 ya upasuaji wa mgongo wamepona na kurudi katika hali zao za kawaida.
NIPASHE
Serikali imeahidi kuifanyia marekebisho sheria ya mikopo itakayosimamia mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini ili kupanua fursa za masomo kwa Watanzania.
Waziri wa Katiba na Sheria Rose Migiro alisema muswada wa Sheria hiyo inatarajia kupitishwa rasmi bungeni Novemba mwaka huu.
Alisema katika bajeti ya Serikali chuo cha Hija hakikua katika orodha ya mikopo endelevu kama inavyopewa vyuo vingine hivyo maboresho ya sheria hiyo yatalenga muendelezo wa mikopo kwa wanafunzi wote.
HABARILEO
Tanzania imeomba Jamhuri ya watu wa China kuongeza idadi ya madaktari inaowatuma nchini kama msaada wa kutuo huduma ya tiba kama njia ya kuwasaidai kukabiliana na upungufu wa madaktari nchini.
Aidha Tanzania imeishauri China kujenga hospitali kubwa inayoweza kulaza wagonjwa100 kwa wakati mmoja wa magonjwa ya moyo na yenye uwezo wa kuwafanyia upasuaji wagonjwa hao.
Rais Jakaya Kikwete alitoa ombi hilo na shukrani zake juzi alipokutana na kuzungumza na Jiang Yikang ambaye ni katibu wa Chama cha Kikomunisti cha China akiwa nchini humo na kuwaomba waendelee kutoa misaada ya tiba kwa Watanzania.
Kikwete pia alishukuru jimbo kwa kuwezesha kujenga hospitali ya moyo Muhimbili.
HABARILEO
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Tanzania EALA Shy-Rose Bhanji amesema tuhumu dhidi yake zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii na magazeti mengine katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo zimelenga kuchafua sifa yake, sababu kubwa akisema ni chuki dhidi ya watu wasiopenda misimamo yake ndani ya bunge hilo.
Katika taarifa yake baadhi ya misimamo yake ni kutetea ardhi ya Tanzania ibaki kuwa mali ya Watanzania pia kumtetea spika wa bunge hilo asiondolewe katika nafasi yake kama baadhi ya wabunge wanavyotaka.
Alisema kutokana na misimamo hiyo amekua akikwaruzana mara kwa mara na baadh ya wabunge wa bunge hilo hivyo sasa wameamua kumtafutia mkakati mwingine wa kumchafua.
Alieleza pia kushangazwa kwake na baadhi ya wabunge kushinikiza madai hayo yajadiliwe bungeni hali iliyosababisha kukwama kikao cha katikati ya wiki iliyopita jijini Kigali kwa sababu ya kutotimia kwa akidi.
HABARILEO
Manispaa ya Kinondoni Dar es salam itaweka kamera za CCTV katika kituo kipya cha mabasi kilichopo Ubungo ikiwa na lengo la kukabiliana na wahalifu mbalimbali wakiwemo wanaoharibu miundombinu.
Mhandisi mkuu Manispaa hiyo Baraka Mkuya alisema madereva wa daladala na abiria wanatakiwa kuwa waangalifu kwa matumizi ya miundombinu ya kituo hicho kwani Manispaa hiyo imepanga kuweka kamera.
Alisema pia ni vyema abiria kutumia vyema miundombinu kwan kituo hicho kilitumia kiasi cha zaidi ya bilioni3.3 ili kiweze kudumu kwa muda mrefu na kuwanufaisha watu wengi.
HABARILEO
Licha ya serikali kusisitiza ugonjwa wa Ebola haujaingia nchini ,hofu ya ugonjwa huo imeendelea kutanda kiasi cha waumini wa kanisa Katoliki Mwanza kulazimika kuomba mwongozo juu ya namna ya kuepuka kugusana wakiwa kanisani.
Hali hiyo ilijitokeza jana wakati Padri Daniel Nana akiwaeleza waumini wake juu ya ujumbe alioupata kuhusu tishio la Ebola Mkoani humo.
Alisema amepokea ujumbe kwa waumini wakitaka mwongozo wa kanisa juu ya utaratibu wa waumini kutakiana amani kwa kupeana mikono wakiwa kanisani.
Alisema utamaduni wa kupeana amani kwa kushikana mikono katika kanisa katoliki umedumu kwa miaka mingi hivyo hauwezi kuzuilika hivyo wasiwe na wasiwasi kwani wanatakiwa kuishi kwa upendo na kumwamini Mungu.
Ni halali yako kupata kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook