Guy Scott ambaye alikuwa makamu wa rais Zambia wakati wa utawala wa Michael Sata ametajwa kushika nafasi ya urais wa nchi hiyo kwa sasa mpaka pale ambapo ataapishwa mara baada ya kufanyika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Waziri wa ulinzi Zambia Edgar Lungu amesema maandalizi ya uchaguzi huo yataanza muda wowote ambapo katiba ya nchi hiyo inaagiza kufanyika uchaguzi wa Rais ndani ya siku 90 baada ya kufariki kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo.
Scott ameteuliwa kushika wadhifa huo ambapo hii itakuwa mara ya kwanza kwa rais mzungu kuongoza nchi ya Afrika tangu kuisha kwa kipindi cha ubaguzi wa rangi Afrika Kusini chini ya utawala wa FW de Klerk.
Kulikuwa na utata uliotokana na katiba ya Zambia kumruhusu Scott kushika wadhifa huo kwa sababu wazazi wake wanatokea Scottland, huku katiba hiyo ikitaja rais wa nchi hiyo ni lazima awe Mzambia kamili kwa maana ya kwamba wazazi wake wote wawili wanapaswa kuwa wamezaliwa nchini humo.