Miaka takribani mitatu baada kuacha kuifundisha klabu ya FC Barcelona, kocha Pep Guardiola amezungumzia kama ikitokea nafasi ya kurudi Nou Camp – atakubali kuifundisha timu hiyo.
Akizungumza na gazeti la Mundo Deportivo Guardiola ambaye alijiunga na Bayern Munich mwaka 2013 baada ya mapumziko ya mwaka mmoja baada ya kuondoka Barca – amesisitiza haoni namna anaweza kurudi kuifundisha klabu hiyo, kwa sababu alishamaliza kazi yake.
Boss huyo wa Bayern Munich alitumia miaka minne Nou Camp – akitengeneza timu ambayo inatajwa kuwa bora kuliko zote katika historia ya soka wakishinda makombe mawili ya ulaya na La Liga mara 3 kuanzia mwaka 2008 mpaka 2012.
Baada ya miezi 12 ya mapumziko, Guardiola aliteuliwa kuwa kocha wa Bayern Munich mwaka jana, japokuwa mara kwa mara imekuwa ikiripotiwa kwamba anaweza kurejea kuifundisha Barca kwa muhula wa pili.
Lakini wakati kocha huyo mwenye miaka 43 akiwa anakiri kwamba atarudi Catalonia kwenda kuishi na mkewe, anasema sio kwenda kuifundisha Barca tena.
“Kwa haraka haraka tu naweza kukwambia kwamba sitoifundisha tena Barca. Naamini kuna maduara kwenye maisha – langu mie na Barca lilishaisha,” aliiambia Mundo Deportivo.
“Mke wangu anafanya kazi jijini Barcelona na wazo ni kurejea tena hapa na kuishi na familia yangu, lakini sijui lini hiyo itakuwa.”