Huku zikiwa zimepita saa chache tangu wawashuhudie mahasimu wao kwenye mbio za ubingwa wa ligi ya Hispania Real Madrid wakipoteza kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi kwa mwaka 2015 , Fc Barcelona walijikuta wakikutana na kichapo kama cha wenzao Madrid baada ya kukubali kipigo cha 1-0 mbele ya Real Sociedad.
Dalili za mwanzo mbaya kwa Barca zilionekana tangu mapema baada ya beki wa kushoto Jordi Alba kujifunga mwenyewe kwa kichwa akiwa kwenye harakati za kuokoa mpira wa krosi uliopigwa toka upande wa kulia .
Bao hili lilidumu hadi mwisho wa mchezo huku Real Sociedad walio chini ya kocha wa zamani wa Manchester United David Moyes wakikomaa na kuwazuia Barcelona katika shambulizi walilopanga .
Pamoja na ukweli kwamba wengi watashangazwa na matokeo haya , ukweli ni kwamba takwimu hazikuwa na ishara nzuri kwa Barcelona kwani mabingwa hawa wa zamani wa ulaya hawajawahi kushinda mchezo wowote kwenye uwanja wa Real Sociedad Estadio Annoetta tangu mwaka 2008 ambapo katika michezo mitano iliyopita walifungwa mara nne huku wakitoka sare mara moja .
Kipigo hiki kimewanyima Barcelona fursa ya kupanda kileleni mwa msimamo wa ligi ya Hispania baada ya kuwashuhudia wapinzani wao Madrid wakipoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Valencia .
Kwa matokeo haya Real Madrid wanaendelea kuongoza ligi wakiwa na pointi 39 wakiwazidi kwa pointi moja wapinzani wao Barcelona wenye pointi 38 sawa na mabingwa watetezi Atletico Madrid japo vijana wa Carlo Ancelotti wana faida ya mchezo mmoja mkononi ambao endapo watashinda wataomgeza tofauti ya pointi baina yao na wapinzani wake wa karibu kwa pointi tatu zaidi .