Mnamo tarehe 12 mwezi huu, macho na masikio ya wapenzi wa soka duniani yataelekezwa Zurich nchini Uswis ambapo kutakuwa na tukio la utoaji wa tuzo za mwanasoka bora wa dunia 2014.
Mshindi wa mara nne mfululizo Lionel Messi, golikipa bora ulimwenguni kwa sasa Manuel Neur na mshindi wa mwaka jana Cristiano Ronaldo watakuwa wanawania kuandika historia nyingine katika ulimwenguni wa soka.
Leo wakati kukiwa na mjadala mkali juu ya nani kati ya watatu hao walioingia kwenye fainali za mwaka huu anayestahili kuchukua tuzo hiyo, kiungo wa FC Bayern Munich Frank Ribery amezungumza juu ya tuzo hizo na namna ambavyo anahisi zipo kisiasa.
Ribery anasema: “Nilijifunza vitu vingi kwenye sherehe za Ballon d’Or mwaka jana. Mara tu nilipofika Uswis, nilimwambia mke wangu kwamba sitoshinda. Kuna siasa nyingi kwenye tuzo ile. Nilimuona Sepp Blatter akiwa anamkumbatia Cristiano Ronaldo na familia yake yote ilikuwepo. Mimi sio mpumbavu, ilikuwa wazi kabisa kwamba lazima ashinde.”
Ribery alikuwa ni mmoja ya wachezaji walioshindwa na Cristiano Ronaldo mwaka jana, ambapo yeye na Lionel Messi walishika nafasi ya pili na ya tatu.