Wabunge wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wanakusudia kupeleka hoja binafsi Bungeni ili kumng’oa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Hawa Ghasia kwa kusababisha vurugu katika uchaguzi na siku ya kuapishwa wenyeviti Serikali za Mitaa.
Akizungumza na waandishi wa Habari jana, Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha CUF, Magdalena Sakaya alisema wameamua hayo baada ya Ghasia mwenyewe kukataa kung’atuka na Rais Kikwete kushindwa kumuwajibisha kwa kushindwa kusimamia uchaguzi.
Sakaya amesema kuna baadhi ya maeneo ambayo uchaguzi haukufanyika lakini CCM ilitangazwa kushinda, huku maeneo mengine ambako vilishinda vyama vya upinzani lakini wakaitwa Wenyeviti waliokuwa wakigombea kupitia CCM kwa ajili ya kuapishwa hali iliyopelekea vurugu.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi Dar wametangaza kumsaka mtu mmoja raia wa Marekani ambaye anatuhumiwa kumuua rafiki yake, Nadine Aburadas ambaye waliyefahamiana miaka mitatu iliyopita kupitia mtandao wa Facebook.
Mtu huyo anatuhumiwa kufanya mauaji hayo katika hoteli Uingereza na kukimbilia Tanzania ambapo vyombo vya habari vya Uingereza viliripoti kuhusu mauaji hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa makosa ya jinai, Diwani Athumani amesema kuwa upelelezi kuhusu mtuhumiwa huyo bado unaendelea wakishirikiana na Interpol japo hana uhakika kama mtuhumiwa huyo bado nchini.
Taarifa zinasema mtuhumiwa huyo aliingia hotelini hapo na marehemu siku ya Desemba 30, siku ya January 1 alionekana akitoka peke yake hotelini hapo, akapanda ndege kwenda Bahrain na baadaye kuja Tanzania.
HABARI LEO
Mfanyabiashara Seleman Manoti amepandishwa Mahakama ya Wilaya Ilala kujibu mashtaka ya kujifanya Ofisa wa Usalama wa Taifa kwa lengo la kudanganya kufanya utapeli maeneo ya Kariakoo, Dar.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na kurudishwa rumande kutokana na kushindwa kwa masharti ya dhamana yaliyomtaka kuwa na wadhamini wawili ambao walitakiwa kulipa sh. mil. 1.
HABARI LEO
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka amesema Jeshi la Polisi Mkoani humo wanamshikilia mwanamke mmoja anayetuhumiwa kusababisha kifo cha mtoto wa mwaka mmoja na mama wa mtoto huyo kulazwa baada ya kunywa pombe ya ‘mturuku’ nyumbani kwa mtuhumiwa huyo.
Kamanda huyo amesema mwanamke huyo mtuhumiwa, Anastazia Kadama aliandaa pombe hiyo ya kienyeji na kuwaalika majirani kumsaidia kulima shamba lake, lakini ikashindikana kwenda kulima kutokana na mvua kubwa kunyesha.
Kutokana na kuhofu pombe hiyo kuharibika aliamua kuigawa kwa watu ili wainywe bure ikiwemo mama ambaye mtoto wake alifariki, Magdalena Muna.
Magdalena aliionja pombe hiyo na kumuonjesha mtoto wake, alianza kutapika na kuharisha, wakiwa njiani kuelekea Hospitali mtoto huyo alifariki.
JAMBO LEO
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Majengo Moshi, Peter Lyimo amelalamikia kuwepo utitiri wa vitabu vingi kwamba vinachangia wanafunzi kufeli katika mitihani yao na kuiomba Serikali kuhakikisha inaweka mitaala inayoendana na maisha ya Watanzania.
Mkuu huyo wa shule amesema kuwa utitiri huo wa vitabu unawachanganya wanafunzi ambao wanashindwa kuchagua vitabu vipi muhimu wasome na vipi wasivisome, huku kukiwa na msululu mkubwa wa vitabu kuingia sokoni bila kuhakikiwa hivyo wanafunzi kusoma vitabu vyenye makosa.
Mwalimu huyo amesema kumekuwa siasa imekuwa ikichangia kwa asilimia kubwa kuvuruga mfumo wa elimu ikiwemo mitaala kubadilishwa mara kwa mara hivyo kuwachanganya walimu na wanafunzi.
Hautopitwa na stori yoyote inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook