Mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Wilfred Bony amekaribia kabisa kujiunga na klabu ya Manchester City baada ya Swansea na mabingwa hao watetezi wa ligi ya England kufikia makubaliano juu ya bei ya mchezaji huyo.
Bony atakuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na City katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili wakati ambapo timu huruhusiwa kusajili wachezaji mpaka dirisha hili litakapofungwa mwezi mmoja baadaye.
Bony atakamilisha usajili wake hivi karibuni ambapo City wamekubali kulipa ada ya uhamisho ya paundi milioni 28 kwa ajili ya mshambuliaji huyo .
Ada hiyo inavunja rekodi iliyowahi kuwekwa wakati kiungo Joe Allen alipouzwa kwenda Liverpool kwa paundi milioni 15 wakati kocha Brendan Rogers alipohama toka Swansea kwenda Anfield.
Manchester City watalipa paundi milioni 25 kwa mkupuo mmoja huku nyongeza ya paundi milioni 3 ikija kutokana na idadi ya mechi atakazocheza Bony na mafanikio atakayopata akiwa na timu yake mpya.
Hata hivyo Bony hataweza kuwa sehemu ya kikosi cha Manchester City kitakachocheza kwenye hatua ya mtoano ya ligi ya mabingwa kwani timu hiyo hairuhusiwi kusajili wachezaji wengine kwa ajili ya michuano hiyo.