Baada ya kusuasua katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya Tanzania bara mpaka kufikia hatua ya kumfukuza kocha Patrick Phiri, hatimaye nyota njema imeanza kuonekana Msimbazi.
Kocha mpya wa Simba SC, Goran kopunovic ameendeleza wimbi la ushindi katika mechi ya sita mfululizo, baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika
Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara jioni ya leo.
Ushindi huo wa pili katika mechi tisa za Ligi Kuu kwa Simba SC msimu huu, unawafanya Wekundu hao wa
Msimbazi watimize pointi 12 na kufufua matumaini ya ubingwa.
Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Mganda, Dan Sserunkuma dakika ya 26 aliyemalizia kwa guu la kushoto kona ya Ramadhani Singano ‘Messi’. Kipindi cha pili, Simba SC ilifanikiwa kupata bao la pili dakika ya 68 kupitia kwa
Elias Maguri aliyemalizia pasi ya Dan Sserunkuma.
Simba SC; Peter Manyika, Hassan Kessy, Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’, Hassan Isihaka, Juuko Murushid, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’/Awadh Juma dk80, Said Ndemla, Dan Sserunkuma/Abdi Banda dk85,
Elias Maguli na Emmanuel Okwi.