Michuano ya kombe la mataifa ya Afrika imeanza rasmi kwa michezo miwili ya kundi A iliyochezwa kwenye siku ya ufunguzi (Jumamosi) ikizihusisha timu mwenyeji Equatorial Guinea na Congo Brazzaville pamoja na mchezo mwingine kati ya Gabon na Burkina Faso.
Katika mchezo wa kwanza Wenyeji Equatorial Guinea na Congo Brazzavile walitoka sare ya kufungana 1-1 katika mchezo uliokuwa mkali na wa kusisimua ambapo timu hizi zilishambuliana kwa karibu dakika zote za mchezo.
Equatorial Guinea ndio walioanza kufunga kupitia kwa nahodha wao Emilio Nsue Lopez ambaye alifunga kwenye dakika ya 16 baada ya kupokea pasi toka kwa Ivan Zarandona.
Timu hizi zilikwenda mapumziko huku wenyeji wakiwa wanaogoza kwa bao hilo moja huku Congo Brazzavile wakimiliki asilimia kubwa ya mchezo.
Katika kipindi cha pili Congo Brazzavile waliendelea na mashambulizi mfululizo na walipata malipo ya juhudi zao baada ya bao safi lililofungwa na mshambuliaji Thievvy Bifouma .
Katika mchezo wa pili Gabon waliendeleza ubabe wao wa siku zote dhidi ya Burkina Faso kwa kuwafunga kwa matokeo ya 2-0 .
Gabon walianza kufunga kwenye dakika ya 19 mfungaji akiwa mshambuliaji na nahodha wa timu hiyo Pierre Emerrick Aubameyang ambaye alifunga kwa shuti la karibu baada ya kuwapita mabeki.
Katika kipindi cha pili Gabon walifunga bao la pili kwenye dakika ya 72 mfungaji akiwa Malick Evouna akimalizia kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Frederic Bulot.
Matokeo haya yanamaanisha kuwa Gabon wanaongoza kundi A baada ya michezo ya kwanza wakiwa na pointi tatu huku Equatorial Guinea na Congo Brazzavil wakifuatia wakiwa na pointi moja kwa kila timu na Burkina Faso wanashika mkia wakiwa hawana pointi yoyote.