Wakati mshambuliaji wa Olympique Marseile, Mario Lemina alipoitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Gabon alikataa katakata na sababu yake ilikuwa moja, hajihesabu kama raia wa Gabon baada ya kuichezea timu ya taifa ya Ufaransa kwenye vijana wenye umri chini ya miaka 20.
Pamoja na kuwa na asili ya Gabon, Lemina aligoma kuichezea Gabon kwani anataka kuiwakilisha timu ya taifa ya Ufaransa na katika hilo anaungana na wachezaji wengine wanaounda orodha ndefu ya wachezaji ambao wakati huu wa michuano ya Afcon labda tungeweza kuwaona wakichezea mataifa ya Afrika badala ya Ulaya.
Tabia hii ya wachezaji wenye asili ya Afrika kuchezea mataifa ya Ulaya haikuanza hivi karibuni, enzi za miaka ya nyuma nyota wawili wa msumbiji Mario Coluna na Eusebio waliondoka nchini mwao wakiwa na umri wa miaka 19 na 18 kwenda nchini Ureno ambako moja kwa moja waliitwa kuichezea timu ya taifa.
Michuano ya AFCON ilianza rasmi mwaka 1957 lakini Msumbiji haikuwa na ligi kipindi hicho na hawakuwa na timu ya taifa ambayo ingeweza kucheza mechi za kimataifa hali iliyosababisha Coluna na Eusebio kuchukuliwa kwenda kuichezea Ureno.
Mchezaji wa zamani wa Barcelona na Glasgow Celtics na Manchester United, Henrik Larson angeweza kuitumikia timu ya taifa ya Cape Verde lakini nafasi hiyo haikuwahi kutokea.
Larson ana asili ya visiwani humo kupitia kwa baba yake mzazi na mwenyewe anakiri kuwa angeweza kuichezea Cape Verde lakini hakuna aliyewahi kuleta wazo hilo na pia alizaliwa na kukulia Sweden hivyo siku zote amejiona kuwa na asili ya taifa hilo la Ulaya.
Timu ya taifa ya Ufaransa imewahi kuwa na wachezaji kama Zinedine Zidane, Marcel Desaily na Claude Makelele ambao ni wazaliwa na Algeria, Ghana na Congo DRC ambayo zamani ilifahamika kama Zaire.
Wengine katika vikosi vya Ufaransa ambao wangeweza kuonekana kwenye AFCON ni Patrick Vieira na Patrice Evra ambao wana asili ya Senegal, Hatem Ben Arfa, Samir Nasri na Karim Benzema ambao wana asili ya Algeria na wengine wengi.
Mfano wa ugumu wa maamuzi kama haya umeonekana kwenye familia ya kina Boateng ambako Kevin Prince na mdogo wake Jerome wamejikuta wakiwakilisha mataifa tofauti, wote wawili wakiwa wameichezea Ujerumani kwenye vikosi vya timu za vijana Kevin Prince aliamua kuichezea Ghana huku Jerome akibaki na Ujerumani ambayo mwaka jana alikuwa moja kati ya wachezaji waliotwaa kombe la dunia wakiwa na timu hiyo.
Nigeria pia imejikuta ikipoteza nafasi ya kuwa na wachezaji nyota kama David Alaba, Stefano Okaka na Angelo Ogbona ambao wote wana wazazi wa kinigeria lakini wamechagua kuichezea Italia sambamba na Mario Baloteli ambaye wazazi wake ni raia wa Ghana lakini leo hii anaiwakilisha Italia sawa na Danny Welbeck ambaye amechagua kuwa raia wa England pamoja na ukweli kuwa wazazi wake ni waghana.
Hakuna Story itakayokupita mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter, instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook