MWANANCHI
Hali bado ni tete kwa mawaziri wakati Rais Jakaya Kikwete akiwasiliana na viongozi waandamizi kabla ya kutangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri baada ya kuwa na vikao kadhaa kabla ya kutangaza mabadiliko wakati wowote, ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kuhusu sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kwenye sakata hilo Anna Tibaijuka aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na kubainika kuingiziwa Sh1.6 bilioni alivuliwa wadhifa huo huku kukiwa na shinikizo kwamba Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo ambaye ni Waziri wa Nishati na Madini kuondolewa pia katika nafasi hiyo.
Rais anatazamiwa kuondoka Jumapili kwenda nje ya nchi kwa safari za kikazi, kwa mujibu wa chanzo cha habari cha gazeti Mwananchi.
Shinikizo kubwa kwa sasa ni kumwondoa Waziri Muhongo, ambaye Rais Kikwete alisema Desemba 22 mwaka jana kuwa amemuweka kiporo kwa siku mbili au tatu kusubiri uchunguzi, lakini mpaka sasa hakuna uamuzi uliofanywa.
Wabunge wa vyama vya upinzani wametshia kumwondoa kwa nguvu mbunge huyo wa kuteuliwa na Rais iwapo atarejea bungeni Jumanne wakati Mkutano wa 18 wa Bunge utakapoanza mjini Dodoma, wakati mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe akisema Bunge halitampa ushirikiano waziri huyo na kwamba atakuwa na kazi ngumu wakati wa Bunge la Bajeti katikati ya mwaka.
Prof. Muhongo anatuhumiwa kutoshughulikia vizuri sakata la Escrow na kusababisha Serikali ikose fedha kwa njia ya kodi. Juhudi zake za kujitetea bungeni ziliishia kwa wabunge kutoa vielelezo kadhaa kuthibitisha hoja za kuhusika kwake kwenye sakata hilo.
MWANANCHI
Wenyeviti wa Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimetangaza kutoshiriki mchakato wa kura ya maoni ya katiba iliyopendekezwa na kuahidi kuhamasisha wananchi kuunga mkono.
Wenyeviti hao Freeman Mbowe (CHADEMA), Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Makaidi (NLD) wamesema wamefikia uamuzi wa kutoshiriki katika zoezi hilo kwa sababu mchakato mzima haukuwa na maridhiano ya kitaifa.
“Vyama vya siasa ikiwemo CCM vilikubaliana mwaka jana kwamba zoezi la kura za maoni lifanyike mwaka 2016 baada ya uchaguzi mkuu, tulisaini wote na Rais Jakaya Kikwete alikubali, kwa nini mabadiliko yafanyike ghafla” – Prof. Lipumba.
“Hadi sasa vifaa vya Biometric Voter Registration (BVR) vilivyopo ni seti 250 wakati vinavyohitajika ni seti 7500, tume inasubiri hadi sasa, zoezi hili litafanyika kweli?,”—Prof. Lipumba.
Aprili 16 mwaka jana, Wabunge wa Bunge Maalum la Katiba kutoka vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD walitoka nje wakidai bunge hilo lilikuwa halijadili maoni ya wananchi yaliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
NIPASHE
Wakazi wa Feri Dar es Salaam wameiomba Serikali kukifanyia marekebisho kivuko cha MV Magogoni kinachofanya safari zake kati ya Kivukoni na Kigamboni ambacho kimekuwa na matukio ya kuharibika mara kwa mara nyakati za usiku na kuchukua muda majini huku kikiwa kimebeba abiria na magari, wengine wakisema kuwa kivuko hicho hakina sifa za kusafirisha abiria wengi na mizigo.
“Abiria tumekuwa na wasiwasi na huu usafiri kwani mara nyingi injini ya kivuko hiki siyo nzima na kusababisha ofu kubwa kwetu,”—abiria.
“Mara nyingi kivuko hiki kikiwa kinafanya safari zake hutumia saa nyingi kufika upande wa pili kutoka na kuelemewa, hivyo kusababisha abiria kutumia muda mrefu kufika kutokana na kutembea taratibu,”– Anna Mwasombe, mwanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
NIPASHE
Jambazi mmoja Njile Samuel maarufu kwa jina la John, amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kulipa faini ya Sh. milioni tatu baada ya kukiri makosa ya kukutwa na risasi 272, bunduki aina ya SMG na magazini saba pamoja na kosa la kumiliki silaha bila kibali.
Wiki iliyopita Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga, walikutana jijini Mwanza na kumuelezea Njile ni jambazi hatari ambaye katika kazi yake amekuwa akiwaua wenzake baada ya kufanya uhalifu.
HABARI LEO
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Monica Mwamunyange amesema Serikali imekubali kuchukua madeni yote ya Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) na kuyalipa, baada ya uhakiki ili kutoa fursa kwa shirika hilo kuanza biashara.
“Shirika hilo litaundwa upya, ikiwa ni pamoja na kumtafuta kiongozi wake kwani Mkurugenzi wa sasa atastaafu mwezi ujao, ikiwa ni pamoja na kupunguza wafanyakazi na kubaki na nguvu kazi yenye tija, kwani kwa sasa tuna ndege moja lakini kuna wafanyakazi 140,”—Monica Mwamunyange.
“Majadiliano na kampuni nne yamekamilika na wamekubali kuondoa gharama zinazofikia bilioni 17.13 katika deni lao,”—Mwamunyange.
Alisema changamoto zingine zinazoikabili ATCL ni ukosefu wa vitendea kazi na wataalamu wa ndege, marubani na wahandisi.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook