Kabla ya mapumziko ya msimu wa baridi, Real Madrid walikuwa wamecheza mechi 22 wakiwa wameshinda zote mfululizo, huku wakiwa wametwaa ubingwa wa dunia pamoja na kuchukua ushindi wa kundi kwenye michuano ya klabu bingwa ya Ulaya.
Ukiwa umepita muda baada ya kipindi hicho mpaka kufikia January 7, tayari Real walikuwa wamepoteza mechi zao mbili za kwanza za mwaka 2015 wakati ligi ya Hispania ikiwa imerejea kwenye ligi na kwneye kombe la Mfalme ambapo walifungwa na Valencia na Atletico Madrid.
Ushindi kwenye mchezo dhidi ya Espanyol ulirudisha timu hiyo kwenye mstari na hadi sasa timu hii inaonekana kurejea kwenye mstari lakini bado haijaweza kurudia kiwango chake bora cha mwanzoni mwa msimu ambapo timu hii ilionekana kuwa kwenye sayari nyingine kabisa.
Tazama ushindi wa tabu kwenye mchezo dhidi ya Cordoba, ushindi uliogubikwa na kadi nyekundu aliyoonyeshwa Cristiano Ronaldo ambapo anajikuta akifungiwa kwenye michezo miwili inayofuatia na utagundua kuwa kuna tatizo mahali.
Kwa wachambuzi wa mambo tatizo hili lilianzia mwishoni mwa mwezi December mwaka jana wakati kikosi cha Real Madrid kiliposafiri kuelekea huko mashariki ya mbali kushiriki michuano ya kirafiki ya Dubai International Sports Conference.
Safari hii ilishuhudia wachezaji wa Real wakihudhuria hafla ya utoaji tuzo ya Globe Soccer Awards huku pia wakishiriki kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya AC Milan.
Pamoja na ukweli kuwa mchezo huu haukuwa na ugumu wowote, Real Madrid walifungwa 4-2 na baada ya hapo timu hii imekuwa kwenye kiwango duni na kama isingekuwa kipigo ilichokipata Barcelona dhidi ya Real Sociedad basi huenda Real wangeondolewa wkenye kilele cha ligi hiyo .
Haikuwa Real peke yao ambao wamekumbwa na upepo huu mbaya, AC Milan nao hawajakuwa kwenye hali nzuri na hii imeonekana zaidi kwenye kipindi kilichofuatia safari yao kuelekea huko falme za kiarabu.
Milan wamejikuta wakianza mwezi januari kwa kuvuna pointi moja pekee katika michezo minne ya mwezi January kwenye ligi kuu ya Italia ikiwa ni rekodi mbaya ya mwanzo wa mwaka tangu miaka 74 iliyopita.
Hadi sasa AC Milan wamejikua wakiwa kwenye nusu ya chini ya Serie A huku ndoto za kufuzu ligi ya mabingwa zikiwa ndoto ya mbali sana mpaka kufikia hatua hii na mbaya zaidi timu hii ilitolewa kwenye kombe la Italia baada ya kufungwa na Lazio katikati ya wiki na kiwango hiki kibovu kimetajwa kuwa mbioni kumhatirishia ajira kocha Philipo Inzhaghi.
Timu nyingine ambayo imeonekana kuathirika na safari ya huko mashariki ya mbali ni Manchester City ambayo katika hali ya kushagaza wengi ilijikuta ikitupwa nje ya michunao ya kombe la FA wiki iliyopita baada ya kufungwa na 2-0 na timu ya Middlesbrough siku tatu baada ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Hamburg Sv huko Abu Dhabi.
City tofauti na wenzao Milan na Madrid hawana faida ya mapumziko kwenye msimu wa baridi kwani ligi ya England haina mapumziko katika wakati huo kama ligi nyingine na kipigo cha Middlesbrough kwenye kombe la FA kilikuja wiki moja baada ya kipigo cha 2-0 dhidi ya Arsenal kwenye ligi kuu ya England.
Inadaiwa kuwa michezo hii inayoziingizia klabu fedha nyingi inaziathiri timu hizi kutokana na urefu wa safari za ndege ambao umeonekana kuwaathiri wachezaji ambao huchoka na kushindwa kuonyesha ubora wao kwenye mechi za ushindani.
Na hili limeonekana dhahiri hasa kwa timu kama Madrid ambayo kimsingi haikupumzika katika kipindi cha majira ya baridi kama wapinzani wao kwenye ligi ya Hispania Atletico Madrid na Barcelona.
Madrid walikwenda nchini Morocco kushiriki kombe la dunia la vilabu kabla ya kwenda Dubai kucheza na Milan na hili linaonekana kuwaathiri sana wachezaji.
Hali hii labda haitadumu kwa muda mrefu lakini lazima klabu hizi zijiulize kwanini zimekumbwa na kiwango hiki kibovu kilichoambatana na matokeo mabaya mara tu baada ya kurudi toka uarabuni ambako walienda kucheza mechi za kirafiki.
Hakuna story itakayokupita mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia twitter instagram na facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook