MWANANCHI
Wabunge wameendelea kuwalipua mawaziri na kumtaka Waziri wa Fedha, Saada Mkuya kufukuzwa kutokana na kukiuka Katiba, huku Mbunge Andrew Chenge akikumbana na kadhia ya kudaiwa kuwa anahusika kwenye kila mikataba mibovu, jambo lililosababisha Chenge kusimama na kutoa kauli ya kutaka ‘kuheshimiana’.
Hayo yalitokea Bungeni Dodoma wakati Wabunge wakichangia taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ya mwaka ulioishia Juni 30 mwaka 2014.
Mkuya alitajwa kubadili matumizi ya fedha zilizotengwa na Serikali kwa ajili ya matumizi mengine, kitendo kinachomaanisha kuwa alivunja Katiba.
“Fedha ambazo ziko kwenye ring fence (mfuko maalumu), hazitakiwi kutumika kwa matumizi mengine kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa Katiba, Waziri umevunja Katiba kwa mujibu wa ibara ya 135 na ibara ya 136 ni Tanzania peke yake (Waziri Mkuya) unabaki salama. Hupaswi hata kupewa heshima ya kujiuzulu, unafukuzwa kazi,” – Esther Bulaya.
Bulaya amekuwa mmoja wa wabunge wachache kutoka chama tawala wanaoihoji Serikali, alisema wizara hiyo imeshindwa kukata fedha kwa ajili ya chai, suti na sambusa na badala yake inakata fedha zilizokuwa ziende kupeleka umeme vijijini.
Wakati wa kuhitimisha mjadala wa ripoti hizo, Naibu Waziri wa Fedha (Sera), Mwigulu Nchemba alikiri kuwa wizara iliyumba katika eneo hilo kutokana na hali ya kifedha ya Serikali.
“Mwaka huu ni hapa tu ambako tuliyumba, (katika) eneo hili la matumizi ya fedha za miradi,” alisema Mwigulu na kuongeza kuwa wizara yake inaandaa utaratibu utakaowezesha makosa hayo kutojirudia.
MWANANCHI
Hofu imetanda kwa wazazi wa watoto ambao wanasoma shule za msingi za Kabasa A na B Wilaya ya Bunda, Mara baada ya kuibuka kwa ugonjwa wenye dalili za kupanda ‘mapepo’ ambao unawaathiri wanafunzi wa kike pekee.
Kutokana na ugonjwa huo kuhusishwa na imani za kishirikina uongozi wa Wilaya uliwataka viongozi wa kijiji kukaa na wazee wa kimila ili kumaliza tatizo hilo.
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya hiyo, Boniface Maiga alisema Serikali haiamini ushirikina, kwa kuwa tatizo limeanzia kwenye jamii basi jamii hiyo hiyo inapaswa kumaliza tatizo hilo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Kabasa B alisema ugonjwa huo ulianza kati ya January 21 na 28 huku wakidhani kuwa ugonjwa huo ni Malaria.
NIPASHE
Sakata la uchotwaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 300 kwenye akaunti ya Tegeta Escrow limeibuka tena bungeni na kuzua malumbano baina ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju na Mbunge Tundu Lissu ambaye alimwambia Masaju kuwa ni mshauri wa serikali na si mshauri wa Bunge kuhusu masuala ya kisheria.
Wakati huohuo Lissu alisema licha ya Bunge kumwondoa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuwafukuza mawaziri, waliochukuliwa hatua ya kufikishwa mahakamani ni watu wadogo waliopewa milioni 80, huku wale waliogawana mabilioni ya fedha wakidunda mitaani.
“Watu wanafanya makosa makubwa dhidi ya umma hakuna hatua inayochukuliwa, waheshimiwa wabunge mnaweza mkauliza, lini mtu amewahi kuwajibika, nani kachukuliwa hatua, yupi amefungwa, tunajua wanajiuzulu ili wakafaidi matunda ya wizi wao, sheria zetu zinasema wajiuzulu, wafilisiwe, washitakiwe na wakipatikana na hatia wafungwe, nani ameshitakiwa, kufilisiwa au kufungwa?”—Tundu Lissu.
Mbunge huyo alisema kuwa Bunge liliazimia majaji waliohusika na sakata hilo Bunge wawajibishwe, lakini Rais Kikwete hajawachukulia hatua kwa madai kuwa majaji hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua na mahakama, huku akishangaa nani anayemshauri Rais masuala ya kikatiba na sheria.
“Maazimio ya Bunge lako ni kwamba serikali ilete taarifa ya utekelezaji maazimio kabla ya kumalizika kwa Bunge la Bajeti lakini hata kabla halijaanza… kanuni zinakataza kumhusisha mheshimiwa Rais kujenga hoja kwa namna ya kejeli, kwa hiyo mimi naomba kushauri kuwa tunapopata fursa ya kuchangia tujikite kwenye hoja yetu na tutumie lugha ya staha kwa sababu ndivyo kanuni zinavyoelekeza,” Mwanasheria Masaju.
Lissu aliongeza kuwa ameipata taarifa ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambaye alimwita mrithi wa Jaji Fredrick Werema huku akimweleza kuwa ni mshauri wa serikali na si Bunge kuhusu masuala ya kisheria ambapo Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu alisimama na kumtaka Lissu kutotumia lugha za vijembe badala yake ajenge hoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Masaju alisimama kuomba mwongozo na kumtaka Lissu kuendelea kuheshimu mihimili mingine kwa kutozungumzia mambo yaliyo mahakamani.
MTANZANIA
Bibi kizee anayekadiliwa kuwa na umri wa miaka 70 asiyejulikana jina wala makazi yake ameanguka akiwa hajavaa nguo yoyote nyumbani kwa mtu mkoa wa Shinyanga jambo ambalo limehusishwa na imani za kishirikina.
Suzana Mwandu ambaye ni mwenye nyumba ambayo kikongwe huyo alianguka anasema alimkuta akiwa nje ya jiko lake ambapo baada ya kumsemesha bibi huyo alizinduka na kuanza kuongea vitu visivyoeleweka ambapo mashuhuda walihisi kwamba ni mshirikina.
Mjumbe wa Serikali ya Mtaa, Waziri Issa amekiri kuwepo kwa tukio hilo ambalo lilikusanya umati wa watu ambapo muda mfupi baadaye Polisi walifika na kumchukua ili kumnusuru bibi huyo kupigwa na wananchi wenye hasira.
MTANZANIA
Mbunge Godbless Lema jana alimshambulia kwa maneno makali Kamishna wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja kuwa anaweza kuwa anashirikiana na majambazi wanaovamia vituo vya polisi na kupora silaha.
Lema aliliambia Bunge kuwa Chagonja anaweza kuwa anahusika katika matukio ya ujambazi katika vituo vya polisi kwa sababu anataka kudhoofisha utendaji kazi wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu huku akifananisha taifa na chumba kinachotumiwa na vijana wa kihuni kuishi ambacho hakina utaratibu.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, geto ni mahali ambapo watu wanaishi bila kufuata utaratibu, yaani katika geto, wakati wa kulala anayewahi ndiye anayelala kitandani. Geto chakula kinapopikwa kinaweza kuliwa hata kama hakijaiva, kwa hiyo nchi hii naifananisha na geto kwa sababu watu wanaiba fedha za umma kama wanavyotaka…” Godbless Lema.
“Katika ripoti za Bunge zilizosomwa hapa jana (juzi) zimejaa wizi, kila ukurasa wa taarifa ya Zitto ni wizi tu, wizi tu, hivi huu wizi utakwisha lini? Hata zile bunduki zinazoibwa katika vituo vya polisi zinaweza kuwa ni ‘sabotage’ (hujuma), zinazofanywa na Chagonja dhidi ya IGP,” — Lema.
Alisema amefanya uchunguzi wake binafsi uliobaini kuwa Jeshi la Polisi limegawanyika na kwamba haamini kama Rais Kikwete amekwishafanya mabadiliko ya uongozi ndani ya jeshi hilo.
Alisema ikitokea mawaziri wa Tanzania wakapelekwa nchini Tunisia wangeishachukuliwa hatua kali kwa sababu Serikali ya nchi hiyo haiwavumilii wabadhirifu wa fedha za umma.
MTANZANIA
Zitto Kabwe ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi na pia Naibu Waziri wa Fedha jana walialikwa kushiriki mahojiano katika kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC) ambapo katika mjadala huo kila mmoja kumsifia mwenzake kwa utendaji kazi uliotukuka.
Katika mjadala huo, Mwigulu ambaye ni mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyeanza kummwagia sifa Zitto kwa jinsi ambavyo amekuwa akitekeleza majukumu yake ya kiuongozi katika nafasi yake ya uenyekiti wa Kamati ya PAC.
Mwigulu alisema Zitto na kamati yake kwa ujumla wamekuwa wakifanya kazi kubwa na nzuri ya kibunge na pia kuishauri vizuri serikali na hasa Wizara ya Fedha.
Zitto alijibu pongezi hizo muda mfupi kabla ya kuhitimishwa kwa mjadala huo kwa kueleza kuwa iwapo Mwigulu ataonyesha nia ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu atamuunga mkono, kwa sababu ameonyesha kuwa ni kiongozi mzalendo na mwenye uwezo mkubwa wa kuelewa matatizo ya wananchi na kuyatafutia ufumbuzi.
Wabunge hao wameonyesha dhamira ya kuunganisha nguvu zao ili kutekeleza malengo yao ya kisiasa, huku kukiwa na mitazamo mbalimbali ndani na nje ya jamii kuhusu wanasiasa vijana waliokwishaonyesha nia ya kuwania madaraka hayo ya juu ya Dola.
Kitengo cha jarida la ‘The Economist’ cha The Intelligence Unit ambacho hufanya ufuatiliaji wa siasa za kimataifa, mwishoni mwa mwaka jana kilimtaja Zitto kuwa ni mmoja wa wanasiasa vijana wa kambi ya upinzani ambaye ana nguvu kkubwa kisiasa.
The Intelligence Unit kilieleza kuwa umaarufu wa kisiasa wa Zitto unatokana na nafasi yake ya kiongozi wa kamati nyeti ya Bunge ambayo imekuwa ikiibua mambo mazito na yenye athari katika taifa, hivyo licha ya kuwa na mgogoro na baadhi ya viongozi wenzake ndani ya CHADEMA, bado anao ushawishi mkubwa wa kisiasa kwa wadhifa alionao ndani ya Bunge.
Hakuna story itakayokupita mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>> twitter Insta Facebook