NIPASHE
Serikali imeruhusu wanafunzi wa shule za msingi na sekondari waliopata ujauzito kuendelea na masomo wanapojifungua.
Mratibu wa Masuala ya Jinsia wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Chimpaye Marango, wakati wa mjadala wa sababu za kuongezeka kwa idadi ya watoto ya mabinti wanaokosa elimu baada ya kupata mimba.
Mjadala huo ulioitishwa na asasi ya kiraia ya uchambuzi wa sera ya Policy Forum iliwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu.
Marango alisema lazima wasichana waliopewa ujauzito kuhakikisha wanarudishwa haraka shuleni mara watakapojifungua, vinginevyo hatua kali watachukuliwa watakaowazuia.
“ Wizara imeliona hilo na tayari imewekwa sera mpya, kwani kumuadhibu kwa kumfukuza shuleni hakutaweza kuwasaidia watoto wa kike kumudu maisha badala yake tunaongeza umasikini ndani ya jamii:- Marango.
Awali, Dk. Rebecca Balira, kutoka Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Tiba Afrika (Amref) alisema tatizo la mimba kwa wanafunzi wa kike limekuwa sugu nchini.
Alisema katika utafiti uliofanyika katika Wilaya za Kilindi, Mkalama, Iringa vijijini na Same jumla ya wanafunzi wa kike 55,000 walishindwa kuendelea na masomo kwa kipindi cha mwaka 2003 hadi 2011.
NIPASHE
Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta, ametangaza kuwashughulikia watu wote waliohusika kulihujumu Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), ambalo ‘limekufa’, huku akionyesha masikitiko yake kuona mpaka sasa hatua kali hazijachukuliwa dhidi yao.
Sitta alisema hayo, wakati akijibu hoja za wabunge, waliochangia mjadala kuhusu taarifa za kazi za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na ya Nishati na Madini, kuanzia Januari 2014 hadi Januari 2015, zilizowasilishwa bungeni jana.
Alisema makosa yaliyotendeka huko nyuma dhidi ya ATCL, ni ya ovyo ovyo kabisa na kushauri Bunge liweke utaratibu wa kutunga sheria za kuwabana watu wanaoyatenda.
Sitta alisema hali mbaya iliyopo ATCL inayotokana na deni linaloikabili, inachangiwa kwa kiasi kikubwa na uzembe unaokaribiana na hujuma.
“Sina hakika kama wahusika wamepatiwa dawa yao. Si ajabu wanatamba tu, wako mahali fulani tu wanaangalia. Basi kuna udhaifu fulani lazima tuurekebishe ili tuweze kwenda vizuri:-Sitta.
Kuhusu usafiri wa treni ya Dar es Salaam, maarufu kama “Treni ya Mwakyembe“, alisema baada ya mkutano kati ya wizara na Wajerumani unaotarajia kufanyika jijini humo, Jumanne ijayo, itaboreshwa zaidi ya ilivyo hivi sasa.
NIPASHE
Mkazi wa Tabata Mawenzi, Remi Joseph (36) anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe kwa kumkata kichwa kwenye nyumba ya wageni ya Friends Corner ya jijini Dar es Salaam.
Aliyeuawa ni Josephena Moshi (35), ambaye alikatwa kichwa na kuchomwa na kitu chenye ncha kali kifuani wakiwa kwenye nyumba ya wageni ya Friends Corner.
Akihojiwa kuhusiana na tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Augustine Senga, alikiri kutokea mauaji hayo.
Senga alisema mwanamke huyo alifariki papo hapo baada ya kushambuliwa na kwamba chanzo cha mauaji hayo hakijafahamika na uchunguzi unaendelea.
Kamanda alipoulizwa kuhusiana na mtuhumiwa huyo kutaka kujiua, alisema kuwa uchunguzi unaendelea.
“Bado ni mapema sana kueleza kila kitu hayo niliyokueleza ni taarifa za awali kwani na huyu mtuhumiwa amekutwa na majeraha shingoni, hivyo masuala ya kazi yake na sababu vinachunguzwa:- Senga.
MWANANCHI
Wakati Serikali ikitafuta njia ya kumaliza tatizo la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi ‘albino’ katika Mikoa ya kanda ya ziwa,imedaiwa watoto ambao hawajafikisha umri na kufariki dunia wakati wa kuzaliwa viungo vyao huuzwa kwa waganga wa kienyeji.
Hayo yalibainika juzi mbele ya Katibu tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mwamvua Jilumbi katika kikao cha pamoja kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT ulioko Bariadi wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati wa kukomesha vifo vya wajawazito.
Wadau hao walibainisha kuwa hali hiyo hujitokeza kila mara katika hospitali ya Wilaya ya Bariadi na walieza pia mtandao wa wahusika wa viungo hivyo hufanyika kati ya wauguzi na madaktari ambao ndio huzalisha wamama wajawazito.
Wadau hao waliendelea kueleza kuwa viungo hivyo vimekuwa vikiuzwa kuanzia 400,000 hadi 500,000.
MWANANCHI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed amesema wananchi hawana imani tena na Jeshi la Polisi kwa kuwa vitendo vya uhalifu vinafanyika, lakini hakuna wanaotiwa mbaroni.
Waziri Aboud alitoa kauli hiyo wakati wa kufunga mkutano wa wakuu waandamizi wa Jeshi la Polisi uliokuwa ukifanyika mjini hapa, huku chombo hicho cha dola kikizidi kurushiwa lawama kutokana na ongezeko la uhalifu ambao umefikia hatua ya vituo vya polisi kuvamiwa na askari kuuawa na kuporwa silaha.
Jeshi hilo pia linalaumiwa kutokana na jinsi linavyoshindwa kushughulikia vurugu kwa weledi na hivyo kujikuta ikitumia nguvu nyingi zinazosababisha wananchi kuuawa na kujeruhiwa.
Waziri Aboud alibainisha kuwa wananchi wengi kwa sasa hawana imani tena na polisi kwa kuwa vitendo vya uhalifu vinafanyika lakini hakuna watuhumiwa wanaokamatwa na kutiwa mbaroni.
“Tabu inakuja pale uhalifu unapotokea na polisi kushindwa kuwapata wahalifu… wananchi wanapenda wahalifu wote watiwe mbaroni na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria:- Aboud.
MWANANCHI
Mbunge wa Bukoba Mjini kwa tiketi ya CCM, Khamis Kagasheki amemtuhumu Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuwa ndiye aliyekuza mgogoro wa Bukoba uliosababisha madiwani wa halmashauri kushindwa kufanya vikao, akidai kuwa mtendaji huyo mkuu wa Serikali ameshindwa kuchukua hatua.
Tuhuma hizo za Kagasheki ni za nadra kwa mbunge huyo wa chama hicho tawala kuelekeza kwa mtendaji mkuu wa Serikali na mmoja wa wajumbe wa vikao vya juu vya CCM.
Kagasheki, ambaye alikuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alitoa tuhumu hizo wakati wa mahojiano maalumu na gazeti hili wiki iliyopita, akisisitiza kuwa ni makosa kuutazama mgogoro huo kuwa ni kati ya yake na meya na akataka ijulikane kuwa kinachoendelea Bukoba ni suala la wizi.
Mgogoro huo wa kisiasa, ambao umedumu kwa takriban miaka miwili na unaotishia kugawanyika kwa CCM, umekolezwa na kufunguliwa kwa kesi tatu ambazo zimezuia utekelezaji wa shughuli za maendeleo na umekuwa ukihusishwa na vita vya ubunge baina ya Kagasheki na Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani.
“Hii ni mara yangu ya kwanza kupata nafasi ya kuzungumzia suala hili. Hakuna unafiki hapa, hili nitalisimamia mahali popote na nitalisema mahali popote kuwa Pinda, ndiye tatizo katika mgogoro huu ulioinyima Bukoba maendeleo:-Kagasheki.
MTANZANIA
Wanakiji wa Namonge mkoani Geita, wameua watu wawili ambao ni askari wa wanyama pori na msaidizi wake, baada ya kuwashambulia kwa mawe, mapanga, rungu na nondo wakiwatuhumu kuwa ni majambazi.
Kufuatia mauaji hayo yaliyotokea wilayani Bukombe, watu 24 akiwamo ofisa mtendaji wa kijiji hicho wanashikiliwa na polisi.
Tukio hilo limetokea juzi jioni baada ya wananchi hao kukusanyana na kuivunja ofisi ya serikali ya kijiji hicho ambako walinzi hao walikuwa wamehifadhiwa na ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Andrea Malise.
Wananchi walioshuhudia mauaji walisema juzi alasiri watu watano, mmoja wao akiwa na silaha aina ya SMG walipita kijijini baadaye kuingia baa wakiwa na pikipiki lakini safari hiyo bila silaha.
Kutokana na kuonekana wageni wanakijiji walianza kuhoji na kuwasiliana juu ya wageni hao.
Pasipo subira inadaiwa wananchi walianza kuwatupia mawe na kuwashambulia ndipo ofisa mtendaji alipoingilia kati na kuwaweka katika ofisi yake kukwepa vipigo kutoka kwa wananchi hao.
Hofu ya wananchi inadaiwa inachangiwa na kuwapo kwa matukio ya kihalifu ya mara kwa mara katika ukanda huo, likiwamo la mnada wa ng’ombe kuvamiwa na watu wenye silaha Januari 16 mwaka huu na wengine wenye silaha kuingia katika kijiji cha Ilyamchele siku tatu baadaye na kuwateka wanakijiji baada ya kuwakirimu.
HABARILEO
WAKATI Jeshi la Polisi likilaumiwa kutokana na namna lilivyoshughulikia maandamano ya Chama cha Wananchi (CUF) wiki iliyopita, Serikali imetahadharishwa kuwa makini na harakati za kisiasa zinazotumia mbinu za kuchokoza Jeshi la Polisi na kuvunja sheria halali.
Wakizungumza na gazeti hili wiki hii kuhusu dhana ya udhaifu wa jeshi hilo, baadhi ya watu wakiwemo wasomi wameitaka Serikali kuwa makini na kauli za wanasiasa, ambao wamewahi kushiriki au kutoa matamko ya kihalifu na leo wanatuhumu jeshi hilo.
Baadhi ya matukio ya kihalifu yaliyotajwa kufanywa katika mazingira ya siasa, tamko la maandamano na migomo isiyokoma, bila kibali cha Polisi, lililotolewa hivi karibuni na Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe na udhalilishwaji wa Mkuu wa Wilaya, wakati wa uchaguzi mdogo wa Igunga uliokuwa na ushindani wa kisiasa mwanzoni mwa 2011.
Tahadhari hiyo imetolewa, wakati Serikali ikielezea kuridhishwa na kazi ya kutunza amani nchini inayofanywa na jeshi hilo, na kuagiza lijiandae na siasa za 2015; siasa za kabla ya Kura ya Maoni ya kupata Katiba Mpya na za kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Maandamano ya CUF Akitoa tamko kuhusu kudhibitiwa kwa maandamano ya CUF wiki iliyopita, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, akizungumzia hoja ya mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia (NCCRMageuzi), kuhusu polisi walivyodhibiti maandamano ya CUF, alisema Prof. Ibrahimu Lipumba, ambaye pia ni Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alikaidi zuio la Jeshi la Polisi.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook