MWANANCHI
Kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa wanafunzi walioshiriki gwaride na halaiki kwenye sherehe za miaka 38 ya CCM mjini Songea ni watoto wa wanachama wa chama hicho, imekosolewa na wananchi na wabunge ambao walifikia uamuzi wa kuomba mwongozo.
Sherehe hizo zilifanyika Jumapili ya Februari Mosi kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, zikishirikisha makundi mbalimbali, wakiwamo wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao walivalia sare za CCM na kuimba nyimbo za chama hicho huku wakicheza gwaride na halaiki, ambayo kwa kawaida huchukua muda mrefu kujifunza na kuielewa.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo, mtendaji huyo mkuu wa Serikali alitetea ushiriki wa watoto hao wapatao 500 kwenye sherehe hizo akisema ni sehemu ya mfumo wa wanachama wa CCM.
“Susan, utafikiri tulikuwa pamoja. Nilijua tu swali hili lazima litaulizwa. Ila ‘mtoto wa nyoka ni nyoka’. Chama hiki kina mfumo wake ambao umeshuka mpaka kwenye ngazi ya kitu kinaitwa chipukizi,” alisema akijibu swali la mbunge huyo aliyetaka kujua sababu za CCM kutumia watoto kwenye shughuli zake za siasa wakati ina wanachama wapatao milioni 10 kote nchini.
“Chipukizi hawa ni watoto ambao wamezaliwa kutokana na wazazi wana-CCM, ndiyo maana chama kiliwatumia. Sherehe ilikuwa nzuri na ilipendeza sana. Kwa kuwa hawajafikia umri wa kuingia katika masuala ya siasa, halina madhara lile rafiki yangu, pia bado ni wadogo mno na walikuwa wanafurahia gwaride na kuvaa sare tu:-Pinda
MWANANCHI
Ziara ya rais wa Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck imeacha mjadala mzito kisiwani hapa kutokana na kitendo chake cha kutumia usafiri wa boti kuja Unguja na kutembea kwa miguu hadi Hoteli ya Serena ya Zanzibar.
Rais huyo, akiwa na mwenyeji wake, Dk Ali Mohamed Shein, alikuwa akitembea mitaa ya Mji Mkongwe, huku akisalimiana na wananchi waliokuwa pembeni ya barabara kushuhudia ujio wake.
Tofauti na viongozi wengi wa juu, Rais Gauck alisafiri kutoka Dar es Salaam kwa kutumia boti ya Kilimanjaro 4 na kuwasili saa 5:30 asubuhi na alipokewa na mwenyeji wake, Shein pamoja na wananchi wakiwamo na wanafunzi.
Baada ya kupigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalum la heshima, kiongozi huyo alianza kutembea huku akisalimia wananchi na wengine kudiriki kuwashika mikono.
Akiwa katika ulinzi wa kawaida, alipita mitaa ya Malindi, Mizigani na Forodhani ambako wananchi walikuwa wamejipanga pembeni huku wakicheza ngoma ya Beni. Siku hiyo maduka yalifungwa kutokana na sababu za kiusalama.
NIPASHE
Wanawake wajane ambao ni Wafugaji jamii ya Kimasai, wamejikuta wakiangua kilio katika kituo cha Polisi Mvomero, mkoani Morogoro baada ya kukabidhiwa idadi pungufu ya ng’ombe zilizokamatwa baada ya kuporwa na kundi la ulinzi wa jadi la wakulima.
Walinzi hao wa jadi kutoka katika kijiji cha Dihombo, lilivamia Kijiji cha Kambala ambacho wanaishi wafugaji hao na kupora ng’ombe 145 kwa madai kuwa wafugaji wa kijiji hicho kuwapora wakulima wenzao pikipiki tatu na kusababisha uhalibifu wa trekta wakati wakielekea shambani katika bonde la Mgongola na pikipiki hizo kutelekezwa porini.
Mmoja wa wanawake hao, Belitha William, alisema akiwa kijijini Kambala akiendelea na shughuli za kuchunga mifugo yake, ghafla alivamiwa na kundi la vijana wenye silaha za jadi maarufu kama muano na kupora ng’ombe wake wapatao 145 pamoja na ndama na kuondoka nao.
Mfugaji huyo alisema alipoifuatilia mifugo hiyo alielezwa inalindwa na kundi la walinzi wa jadi mpaka pale wafugaji wa jamii hiyo ya kimasai watakaporudisha pikipiki walizopora wafugaji wenzao.
Hata hivyo, alisema baadaye mifugo hiyo ilipelekwa ofisi ya Tarafa ya Mvomero kwa ajili ya kupigwa faini mifugo hiyo kuzurura katika mashamba huku mingine ikiwa haipo.
Kwa upande wao, wakulima walioporwa pikipiki hizo, Fabian Clement pamoja na Francis Boniface, wakielezea tukio la kuporwa pikipiki hizo, walisema kwa nyakati tofauti kuwa wakati wakielekea katika mashamba ya bonde la Mgongola kwajili ya kuwapelekea chakula wenzao, waliona kundi kubwa la wafugaji jamii ya Wamasai wakiwa na silaha za jadi pamoja na bunduki likiwafuata ndipo walipokimbilia porini.
MTANZANIA
Wazir Mkuu wa Zamani Edward Lowassa, amekanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la kila wiki iliyosema “Lowassa apanga safu”, akisema hana haja ya kufanya hivyo wala kutumia fedha kumnadi mgombea yeyote.
Taarifa iliyotolewa ofisi yaje jana, ilisema habari hiyo ilijengwa na taswira ya uongo kwamba kuna mpango wa kupanga nani atagombea ubunge katika Jimbo la Monduli baada ya Lowassa kumaliza muda wake.
“Taarifa hiyo potofu ilikuwa na lengo la kumshushia Lowassa hadhi kwa wananchi wake,” ilisema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Lowassa anatarajia kupeleka malalamiko rasmi kwenye Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Idara ya Habari (Maelezo) ili ukweli ujulikane.
Ilisema habari hiyo ilidai kuwa Lowassa amewahonga makada kadhaa wa CCM wilayani humo ambao wameonyesha au wana nia ya kuwania kiti hicho, Sh millioni 10 kila mmoja ili wamuunge mkono Mbunge wa Viti Maalum, Namelok Sokoine.
MTANZANIA
Mtuhumiwa Tissi Mallya ambaye alitoroka baada ya kumuua polisi, G.7168 Koplo Joseph Swai, ameauwa usiku wa kuamkia jana na wananchi alipokuwa amejificha akiwa na panga lenye damu lililotumika kwenye mauaji hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) David Misime alisema hayo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Mauaji hayo yalitokea juzi asubuhi katika eneo la Chang’ombe Juu.
Kamanda Misime alisema baada ya Malya kutekeleza mauaji hayo alikimbia lakini ilipofika saa 5.00 usiku wananchi walimuona maeneo ya Mtimkavu Mailimbili akiwa bado na panga alilotumia kumuua Koplo Joseph.
“Wananchi walichukua sheria mkononi na kumshambulia hadi polisi walipofika eneo la tukio wakamchukua na kumkimbiza katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma lakini aligundulika tayari amekwisha kufariki dunia:-Misime
HABARILEO
TANI 200,000 za silaha haramu zilizokuwa zimezagaa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) zimeteketezwa.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu wa EAC, Richard Sezibera mbele ya Rais wa Shirikisho la Ujerumani, Joachim Gauck wakati alipozuru makao makuu ya jumuiya hiyo, jana.
Alisema silaha hizo zilizokamatwa kwa nyakati tofauti katika nchi mbalimbali za EAC ni pamoja na mabomu tani 200.
Akizungumzia ujio wa Rais wa Ujermani katika makao makuu ya Jumuiya hiyo, Sezibera alikiri kufurahishwa na ujio huo na kusema kuwa utaongeza chachu ya nchi hiyo kuisaidia jumuiya hiyo.
Sezibera alisema mahitaji makubwa yanahitajika katika kufanikisha mahitaji ya wananchi wa EAC ikiwa ni pamoja na Afya, Mazingira, Miundombinu na vikundi vya akina mama na vijana wanachama wa jumuiya hiyo.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook