MWANANCHI
Gazeti la Mwananchi limethibitisha kuwa Rais Kikwete alianza kuongoza nchi mwaka 2005 kwa kuteua jumla ya mawaziri na manaibu 60, anaondoka akiwa ameteua jumla ya watu 118 kushika nyadhifa hizo kwa mabadiliko ambayo yamefanywa jumla mara tatu.
Rais Kikwete alitangaza baraza lake la kwanza kwa kuteua mawaziri 29 na manaibu 31, idadi ambayo ilikuwa kubwa kulinganisha na marais waliopita, alipofanya mabadiliko ya kwanza makubwa mwaka 2008, alipunguza idadi kwa kuteua mawaziri 26 na manaibu 21 huku ikitajwa kuwa idadi kubwa ya walioteuliwa kuwa mawaziri, ilichangiwa na mabadiliko lilipovunjika baraza mwaka 2008 kutokana na Edward Lowassa kujiuzulu uwaziri mkuu.
Mabadiliko ya kwanza ilikuwa 2008 kutokana na ishu ya RICHMOND iliyosababisha Lowassa kujiuzulu na baadaye mwaka 2012 kutokana na kashfa iliyotokana na ripoti ya CAG na mwisho ilikuwa 2014 iliyotokana na kashfa ya Operesheni Tokomeza.
“Mabadiliko haya ninayachambua katika sehemu mbili. Kwanza, ili mtu aweze kufanya kazi kwa utulivu na kutekeleza mikakati yake ni lazima awe na muda wa kutosha. Kama akikosa utulivu taasisi (wizara) aliyopo inaweza kuyumba,” alisema Mkuu wa Shule ya Sheria wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Profesa Bonaventure Rutinwa.
“Ili kuepusha jambo hili. Uteuzi katiza wizara kama hii ya Nishati na Madini unatakiwa kufanywa kwa umakini zaidi ili kuepuka kubadili mawaziri mara kwa mara. Kama waziri anakuwa na mipango ya muda mrefu na akaondoka ndani ya kipindi kifupi, mambo yanaweza kukwama,” Prof. Rutinwa.
“Uwaziri utaendelea kuwa wako iwapo tu utafanya vizuri kazi zako. Hata Rais Kikwete wakati akiingia madarakani aliwahi kusema wazi kuwa yeye na Makamu wa Rais ndiyo wenye nafasi za kudumu, si mawaziri aliowateua,” Prof. Rutinwa.
MWANANCHI
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imetajwa katika utafiti kuwa ni kati ya taasisi zilizoshika nafasi za juu kwa kupokea rushwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Utafiti huo unaoitwa ‘Baada ya muongo mmoja wa kupambana na rushwa, tumepiga hatua kiasi gani?’ umefanywa na Taasisi ya AFROBAROMETER ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na REPOA na ulifanyika kati ya Agosti 26 hadi Septemba 29, 2014 kwa kuwahoji watu 2,386 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.
“Mambo yanafanyika lakini hayawafikii watu wa chini. Walipenda kusikia fulani kapelekwa mahakamani. Watu wanaweza kusema taasisi fulani kuna rushwa kwa sababu kuna vitu fulani havijafanyika,” alisema Mosha ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma wa Takukuru.
Hata hivyo mkurugenzi huyo alisema kama utafiti huo ungefanyika Oktoba mwaka jana, anaamini matokeo yangekuwa tofauti kwa namna taasisi hiyo ilivyolishughulikia suala la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema baadhi ya watu wanailaumu TAKUKURU bila kufikiri kuwa taasisi hiyo haina nguvu ya kisheria ya kutekeleza mambo inayotaka.
Matokeo ya utafiti huo yamebainisha kuwa 64% ya wananchi waliohojiwa walisema kuwa rushwa inazidi kuongezeka nchini huku 29% ya wananchi waliohojiwa walisema kuwa maofisa Takukuru wanapokea rushwa ikiwa ni ongezeko la asilimia moja ikilinganishwa na matokeo ya utafiti kama huo uliofanywa mwaka 2012.
Matokeo ya utafiti huo pia yanaonyesha 50% ya waliohojiwa wanasema kuwa Jeshi la Polisi linaongoza kwa kupokea rushwa nchini wakati maofisa wa TRA wanafuatia kwa 37%, majaji na mahakimu 36% na maofisa wa Serikali za Mitaa asilimia 25%.
HABARI LEO
Mbunge David Kafulila ameshindwa kuwasilisha hoja binafsi, kuitaka Serikali iwasilishe bungeni ripoti ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), kuhusu uchunguzi wa tuhuma za rushwa katika sakata la iliyokuwa Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kafulila amesema ilikuwa kuwezesha Bunge kufanya uamuzi mwingine wa alichoita ni uchunguzi mpana na wa kina.
Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na Bunge kwenda kwa mbunge huyo, ambayo gazeti la HABARI LEO lilipata nakala yake Bunge limezuia hatua hiyo ya Kafulila kwa sababu ilikuwa inakiuka Kanuni za Bunge.
Barua hiyo ilieleza kuwa suala hilo lilijadiliwa na kuhitimishwa na Bunge katika mkutano wa 16 na 17 na kutolewa maazimio yanayotakiwa kutekelezwa na serikali, ikiwa ni pamoja na Takukuru.
Kafulila alisema ripoti iliyojadiliwa awali ilikuwa ya CAG, ambayo inaangalia upungufu wa kisheria, lakini Takukuru wanajadili mpaka kesi za jinai ambapo ,mjadala huo ungewezesha kuwekwa wazi watuhumiwa kwa asilimia 70, wakati ile ya CAG ni asilimia 30 tu.
Kafulila alisema baada ya kuzuiwa kutoa hoja yake binafsi, anajadiliana na wanasheria wake kuangalia taratibu za kikanuni ndani ya mamlaka ya Bunge, ili kupata ushauri nini cha kufanya.
Kuhusiana na ishu hiyo, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka aliondolewa katika nafasi yake pamoja na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Frederick Werema na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo kujiuzulu.
RAIA TANZANIA
Walimu wa shule za msingi na maofisa Elimu Lindi wamesema kuwa suala la wazazi kutotambua umuhimu na faida ya elimu imetajwa kuwa moja ya sababu ambacho zinachangia utoro wa wanafunzi.
Mwalimu Mkuu shule ya Kisiwani Siwema Milanzi amesema kuwa wazazi huwachukua watoto wao na kuwapeleka kufanya kazi za uvuvi, biashara na wengine huozeshwa, hukuwazazi wengine wakiwashawishi watoto wao kufanya vibaya masomoni ili wasiendelee na masomo.
NIPASHE
Joseph Minja (66) mstaafu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege aliyekuwa akiishi Mbezi, Dar amekutwa akiwa ameuawa na watu wasiofahamika na mwili wake kuwekwa ndani ya friji kwenye nyumba yake, mwili wake ulibainika siku ya pili baada ya tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Kinondoni Camilius Wambura amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi.
Jirani mmoja wa Minja aliyeongea na gazeti la NIPASHE amesema alipokea simu kutoka kwa mfanyakazi wa baa ya marehemu iliyo jirani na nyumba yake akimtaarifu kwamba jana yake usiku walivamiwa na majambazi lakini yeye alifanikiwa kutoroka baada ya kukatwa panga la mkono.
Kijana huyo alimtaka jirani huyo kwenda kuangalia nyumbani kwa mzee Minja kuna hali gani, walipochungulia dirishani walikuta mguu wa mtu ukiwa unaning’inia kutoka kwenye friji ndipo wakatoa taarifa Polisi.
Jirani mwingine amesema baada ya Polisi kufika walikuta bomba la sindano lililotumika pamoja na dalili za kuchimbwa pembeni ya karo ambapo wanahisi huenda walikuwa wakitaka kuuficha mwili wa mzee huyo.
MTANZANIA
Wilaya ya Tarime imetajwa kuongoza kwa vitendo vya ukeketaji ambapo kwa 2014 watoto takribani 1,400 wamefanyiwa ukeketaji kwa mujibu wa Ripoti ya LHRC .
Mkurugenzi wa LHRC, Harold Sungusia amesema matokeo ya utafiti huo ambao umeshirikisha na asasi nyingine umeonesha kuwa 15% ya watoto Tanzania wamekeketwa huku kukiwa na changamoto kubwa ya mapungufu kwenye Sheria ya Ukeketaji ambayo inawalinda watoto wa miaka 18 pekeyao pamoja na kikwazo cha ushirikiano mdogo wanaoupata kutoka Jeshi la Polisi.
Sungusia amesema mwaka huu wamepanga kutoa elimu kwa wauguzi nchi nzima ili wajue athari za ukeketaji.
HABARI LEO
Tanzania imeingia mkataba wa kubadilishana wafungwa kwa nchi za Thailand na Mauritius ambapo hadi sasa Tanzania imeweza kupokea wafungwa kumi kutoka nchi hizo kutekeleza mkataba huo.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima aliongeza kuwa katika kutekeleza mkataba kati ya kubadilishana wafungwa hao 10, tisa wameshamaliza hukumu za vifungo vyao huku mmoja anategemea kumaliza kutumikia kifungo mwaka 2021.
“Mpaka sasa Serikali yetu imeweza kuhudumia wafungwa kumi kutoka nchi hizo mbili ambapo mwanamke mmoja na wanaume tisa”—Naibu Waziri Silima.
Naibu Waziri huyo amesema Serikali iko katika mkakati wa kusaini mkataba na nchi nyingine tatu, Kenya, China na India ambako kuna wafungwa wengi wanaokabiliwa na kesi za dawa za kulevya.
Silima amesema kwa wafungwa ambao Tanzania haina mkataba wa kubadilishana wafungwa, wawasiliane na balozi za Tanzania ili kupata msaada wa kisheria.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook