MWANANCHI
Waendesha bodaboda sasa wanaweza kufananishwa na ‘Serikali’ inayojitegemea au taasisi ya kipekee kutokana na kuunda umoja katika ulinzi na usalama, biashara, vizazi na hata katika vifo na magonjwa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa hivi sasa waendesha bodaboda wana utawala wao, unaowaongoza katika maeneo mbalimbali.
Inapotokea ajali kati ya dereva wa gari na mwendesha bodaboda baada ya dakika chache, kundi la waendesha bodaboda litafika na kuanza kumwadhibu dereva wa gari na imebainika kuwa umoja huu unatokana na waendesha bodaboda kuwa na imani kuwa wanagongwa kwa makusudi au pengine ni njama za kuwaua na kuwakomoa.
Mara kadhaa waendesha bodaboda wameonekana wakiandamana pale inapotokea mwenzao amegongwa na gari, kuibiwa pikipiki au kufanyiwa jambo lolote lile.
Katika vituo vingi vya bodaboda, imegundulika kuwa licha ya kuwa na uongozi kwa mfano Mwenyekiti, na Katibu, lakini kuna polisi wa kituo.
“Polisi kazi yake kuangalia kuwa mwenzetu yupo salama, wakati mwingine mwenzako anakodiwa halafu hajarudi mpaka jioni lazima umpigie simu,” alisema Mwenyekiti wa waendesha bodaboda wa Kimanga, Said Kuleka.
MWANANCHI
Wapo wastaafu wengi wa Serikali ambao wanafuatilia kwa karibu nyendo za siasa nchini, mmoja wapo ni Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa (68) ambaye amekitahadharisha chama cha CCM kwamba kijiandae kwa Serikali ya mseto.
“Na endapo Rais atatoka CCM na wabunge wengi ndani ya Bunge wakawa ni wa upinzani, basi lazima Rais huyo akubali kufanya kazi na upinzani.
“Itabidi akubali kuunda Serikali ya mseto, japo sitarajii kufika huko. CCM ni imara, lakini tuwe na fikra hizo pia kwa nia nzuri ya kuiweka nchi katika amani,” ni kauli ya Kanali Mjengwa ambaye pia ni mkuu wa wilaya mstaafu.
Kanali Mjengwa alisema licha ya upinzani kuwepo na kujipambanua kwa wananchi, lakini bado siyo tishio kwa CCM na itaendelea kushika dola tu kwani inaaminika na Watanzania wengi.
“Upinzani kuingia Ikulu bado sana, ila kwenye nafasi ya ubunge na udiwani ndiko kutakuwa na changamoto kubwa. Kuna uwezekano mkubwa wa wabunge wengi wakatoka upinzani lakini siyo Rais.
“Lakini niseme tu kwamba pamoja na CCM kuendelea kuaminiwa na wananchi wengi, isibwete wala kupuuza upinzani. Hawa jamaa wanazidi kujitanua kweli kweli, hivyo wanaweza kuiyumbisha:- Mjengwa.
Kanali Mjengwa alisema CCM bado inaaminiwa na Watanzania wengi, lakini tatizo linalomkera na mabalo kwa maoni yake linaharibu adabu na sifa ya CCM ni kitendo cha wana-CCM kuchafuana majukwaani.
MWANANCHI
Waombolezaji kwenye msiba uliotokana na ajali ya moto ulioteketeza watu sita wa familia moja, wamelaumu Kikosi cha Zimamoto cha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kushindwa kufika kwa wakati eneo la tukio.
Juzi familia ya watu sita ya Mzee David Mpira na mkewe Celina, iliteketea kwa moto ikijumuisha Lucas Mpira, Samwel Yegela, Pauline Emmanuel na Celina Emmanuel. Chanzo cha moto huo inadaiwa kuwa ni hitilafu ya umeme.
Katika tukio hilo, Emmanuel Mpira ndiye pekee aliyenusurika katika ajali hiyo kwa kuwa wakati moto unatokea yeye alikuwa ametoka kwenda matembezini.
Jana, waombolezaji hao ambao wengi ni wakazi wa Kipunguni A ilipoteketea nyumba hiyo, kwa nyakati tofauti walisema hakuna haja ya kuwepo kikosi hicho ambacho mara kwa mara kimekuwa kikifika kimechelewa kwenye maeneo ya matukio ya ajali na hata kama wakiwahi wanakuwa hawana maji. “Tumepiga simu tangu saa 10.00 usiku mara baada ya kuona moto unateketeza nyumba lakini wamefika hapa saa 12.00 asubuhi wakati moto umeshateketeza kila kitu,” alisema Abdallah Mlele mkazi wa eneo hilo.
Akizungumzia hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi Maalumu, Prof. Mark Mwandosya ambaye ni ndugu wa familia hiyo, alisema si vizuri kuzungumzia suala hilo katika kipindi hiki bali kinachotakiwa ni kusubiri uchunguzi.
“Huwezi ukawalaumu zimamoto kwa sasa, au Tanesco kutokana na hili, tusubiri uchunguzi ndipo tupate pa kuzungumzia,” alisema.
NIPASHE
Katika hali inayoweza kutafsiriwa kama ‘sarakasi’, bei ya sukari imepanda ghafla kwenye maduka ya jumla na rejareja jijini Dar es Salaam na mikoani.
Uchunguzi umebaini kuwa, bei ya jumla ya sukari ya ndani yenye uzito wa kilo 50, imepanda kutoka Sh. 64,000 hadi Sh. 88,000 mpaka Sh. 100,000 kwa jijini Dar es Salaam, wakati mikoani bei hiyo imepanda kutoka Sh. 64,000 hadi Sh. 88,000.
Mkoani Kilimanjaro, mjini Moshi, bei ya rejareja ya sukari ya kiwanda cha Moshi (TPC) ni Sh. 2,000 kwa kilo moja.
Baadhi ya wafanyabiashara wa sukari walisema sababu za kupanda kwa bidhaa hiyo ni baada ya serikali kuzuia uangizaji wa sukari ya nje.
Katika maduka ya jumla eneo la Manzese na Kijitonyama, mfuko wa sukari ya Kilombelo wa kilo 50 ulikuwa unauzwa kuanzia Sh. 88,000 hadi Sh. 90,000 wakati bei ya awali ilikuwa Sh. 62,000
Kadhalika sukari ya kilo 20 inauzwa Sh. 36,000 wakati bei ya awali ilikuwa Sh. 31,000.
NIPASHE
Mahakama ya Wilaya ya Chato, mkoani Geita, imewahukumu kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja, Joseph Christopher (25) mkazi wa kijiji cha Nkome na Bahati Juma (28) mkazi wa Katoro wilayani Chato, baada ya kuwatia hatiani katika shitaka la kujifanya maofisa wa polisi kwa lengo la kufanya utapeli.
Katika kesi hiyo, washitakiwa hao walidaiwa kufanya utapeli katika kijiji cha Buseresere, Septemba 4, mwaka jana na kujipatia simu mbili za mkononi pamoja na Sh. 11,000 taslimu kinyume cha sheria.
Katika hati ya mashtaka, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chato, Alex Mukama, aliieleza mahakama kuwa, washitakiwa hao walitenda kosa hilo kwa lengo la kujipatia mali hizo baada ya kujitambulisha ni maofisa wa Jeshi la Polisi na kwamba wametumwa kijijini hapo kufanya upelelezi wa wahalifu.
Alidai baada ya kutumia ulaghai huo, washtakiwa hao walichukua simu za mkononi za vijana wawili pamoja na fedha Sh. 11,000 kisha kutokomea na kuwaacha vijana hao wasijue la kufanya.
Alieleza hata hivyo, vijana hao walifanikiwa kumuona mmoja wa washtakiwa hao akiwa kituo cha mabasi na kuanza kupiga yowe la kuomba msaada, ambapo alikamatwa na kufikishwa kituo cha polisi Buseresere.
NIPASHE
Mbio za kuusaka urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), zimezidi kupamba moto baada ya kundi la wabunge wapatao 150 kujitokeza hadharani na kueleza kumuunga mkono mmoja wa wanaotajwa kuwa wagombea, Edward Lowassa, wakimtaka kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Hali hiyo inajitokeza wakati wa Mkutano wa Bunge wa 18 ukihitimishwa mwishoni mwa wiki na kubakia miwili tu Bunge la 10 kufikia tamati, hivyo kwa kila hali uchaguzi mkuu kuzidi kunukia kazi kubwa ikiwa ni kupatikana kwa rais wa tano wa Tanzania.
Kwa kitambo sasa kumekuwa na makundi yanayosigana kila moja likiwa na mgombea wake, hata hivyo mpambano mkubwa wa kumpata mgombea unaonekana kuwa zaidi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kurithi mikoba ya Rais Jakaya Kikwete, anayehitimisha uongozi wake wa utawala Oktoba mwaka huu kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika mbio hizo, sasa ni rasmi kwamba kundi la wabunge wanaodaiwa kufikia 150 walikutana katika chakula cha jioni mjini Dodoma eneo la Kilimani mwishoni wiki iliyopita wote waliopata fursa ya kuzungumza katika hafla hiyo, walisema wazi kuwa wanamuunga mkono Lowassa katika mbio za urais.
Lowassa ambaye pia ni mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, anadaiwa kutakiwa na wabunge hao kuwa muda ukifika achukue fomu za kuwania urais kwa tiketi ya CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Ingawa kumekuwa na tetesi na minong’ono ya Lowassa kuungwa mkono ndani ya CCM kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa ambayo pia itampa fursa ya kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, uamuzi wa wiki iliyopita wa wabunge hao kusimama hadharani unaibua moto mkubwa wa kinyang’anyoro cha urais huku jina la Lowassa likizidi kutajwa kama chaguo la wengi.
MTANZANIA
WASICHANA 22 walioingizwa nchini na mmiliki wa Continental Night Club na Hunters Club, Omprakash Singh kwa ajili ya kufanya biashara ya ukahaba wanarudishwa leo Nepal na India walikotoka.
Akizungumza jana na Mtanzania kwa njia ya simu, Kamishna wa Uhamiaji Udhibiti na Usimamizi wa Mipaka, Abdallah Abdullah, alisema wasichana hao wanatarajia kuondoka leo baada ya kumaliza matibabu waliyokuwa wakipata.
“Wasichana waliokuwa wanaugua TB na UTI wote wamepona, tiketi zilichelewa kidogo lakini zimepatikana wanasafiri kesho (leo),”alisema.
Alisema Singh ameshalipa faini ya Sh milioni 15 alizoamuliwa kulipa na mahakama, pamoja na kulipa mishahara ya wasichana hao Dola za Marekani 30,625.
HABARILEO
Shirika la Utafiti wa Maendeleo ya Elimu (TEDRO), limesema katika utafiti walioufanya kuhusu ushiriki wa vijana katika siasa na matarajio kuelekea uchaguzi mkuu 2015, umeonesha kwamba endapo mgombea urais kijana atapendekezwa atakubalika kwa asilimia 82.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa shirika hilo, Jacob Kateri alisema katika wananchi hao waliohojiwa pia asilimia 11 walisema vijana hawatakubalika na asilimia saba walisema hawajui.
Alisema utafiti huo umeandaliwa na kufanyika Tanzania Bara na maeneo yaliyohusishwa ni kanda za kijiografia ili kuwezesha uhusishwaji mpana wa Watanzania na katika kila wilaya wamehojiwa wananchi wa vijiji vitatu kwa kuzingatia siasa za eneo husika.
Aidha alisema utafiti huo umeonesha sababu mbalimbali zinazoweza kuwa kichocheo cha vijana kuingia katika siasa ambapo zilizochukua uzito ni uzalendo kwa asilimia 67 ambapo wananchi walisema vijana wengi wameingia katika siasa kwa sababu ya uzalendo.
“Sababu nyingine ni kimbilio baada ya kukosa ajira kwa asilimia 57, uwezo mdogo wa watangulizi wao katika nafasi husika kwa asilimia 60, mafanikio ya wanasiasa vijana walio mahiri asilimia 72, vyama vya siasa kuwapa nafasi vijana katika vyama vyao kwa asilimia 59 na kukubalika kwa vijana kwa asilimia 63:-Kateri.
Aidha alisema wanasiasa vijana waliopendekezwa kupitia chama tawala aliyeoonekana kuongoza kwa kukubalika ni Mwigulu Nchemba kwa asilimia 38, Dk Emmanuel Nchimbi kwa asilimia 26, January Makamba kwa asilimia 24, William Ngeleja kwa asilimia 11 na Lazaro Nyalandu kwa asilimia 10.
Wengine ni Hamisi Kigwangala kwa asilimia saba, Deo Filikunjombe kwa asilimia tano, Esther Bulaya kwa asilimia 2 na waliosema hakuna anayefaa walikuwa asilimia 9 na asilimia 13 walipendekeza wengine wasio vijana.
Utafiti huo pia unaonesha kwamba kijana anayepewa nafasi kubwa endapo atasimamishwa kupitia upinzani anayeongoza ni Zitto Kabwe kwa asilimia 18, James Mbatia kwa asilimia 16, Tundu Lissu kwa asilimia 14, Halima Mdee kwa asilimia nne na David Kafulila kwa asilimia sita.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook