Sakata la mauaji ya Farahan Maluli, anayedaiwa kuuawa na rafiki yake ambaye ni mtoto wa bosi wake, limezidi kuchukua sura mpya baada ya mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi mtuhumiwa wa mauaji hayo, Hemed Hamis, kusimulia jinsi alivyomuomba kusakafia uani baada ya mauaji hayo kufanyika.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mmiliki wa nyumba hiyo iliyopo eneo la Ilala Sharif Shamba, Amjad Zahor, alidai kuwa baada ya kulipa fedha za pango la nyumba awamu ya pili, alianza kulalamika kuwa mfumo wa kupitishia maji taka haukuwa mzuri kutokana na kujaa maji kipindi cha mvua.
Zahor alidai kwamba kutokana na hali hiyo, mpangaji wake ambaye ni Hemed (mtuhumiwa), aliomba alete gari kwa gharama zake kwa ajili ya kunyonya maji machafu, lakini alikwama kutokana na matope kuwa mengi. Baada kazi hiyo kushindikana, Hemed alimweleza mmiliki wa nyumba kuwa hatagharimia tena kukodi gari badala yake atachukua vijana wamsaidie kutoa matope hayo.
Zahor alidai kuwa baada ya hapo, mtuhumiwa wa mauaji (Hemed), aliamua kusakafia uani ili matope yasiendelee kuingia kwenye mfumo wa maji taka.
“Hali hiyo haikunishtua kwa kuwa nilielezwa tangu awali kinachotaka kufanywa na mpangaji wangu:- Zahor.
Alisema baada ya kusakafia nyumba hiyo, Hemed alihama katika nyumba hiyo Septemba, mwaka jana bila kutoa taarifa.
Zahor alidai kwamba katika mazungumzo yao, mtuhumiwa alimuomba wapigiane hesabu kujua kiasi cha fedha anazodai baada ya kuhama kabla ya kwisha muda wa mkataba waliokubaliana.
NIPASHE
Rubani wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), Reney Petersen (28) na mwenzake, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka manne ya uhujumu uchumi.
Pia wanatuhumiwa kuingiza mitambo na kuingilia mawasiliano ya simu za kimataifa bila kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni moja.
Rubani huyo ambaye ni Mtanzania mwenye asili ya Uholanzi na mwenzake Jerry Diaz (25) walisomewa mashitaka yao mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Janeth Kaluyenda.
Wakili wa Serikali Janeth Kitale alidai kuwa siku isiyofahamika mwaka 2014 washtakiwa huku wakijua ni kosa kisheria, waliingiza nchini mitambo ya kielektoniki ya mawasiliano bila kuwa na leseni ya TCRA.
Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa siku isiyofahamika jijini Dar es Salaam, washtakiwa walisimika mitambo ya kielektoniki ya mawasiliano bila kupata leseni ya TCRA.
NIPASHE
Mwenyekiti wa chama cha ACT -Tanzania, Kadawa Limbu, amemshambulia kwa maneno hadharani Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, kwa madai kuwa anambeba Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba na amekuwa chanzo cha migogoro ndani ya vyama vya siasa.
Limbu alianza mashambulizi hayo jana wakati wa mapumziko mafupi katika mkutano wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na vyama vya siasa, kwa kudai kuwa yeye ndiye aliitisha mkutano halali na wanachama halali, huku Mwigamba akiwa na wanachama ambao siyo halali.
“Kweli hivi ndivyo unavyosimamia vyama vya siasa?, nimefika hapa nashangaa kumuona Mwigamba, siyo sahihi kabisa,” alisema na Msajili alimuuliza: “Umepata barua yangu na umeisoma?”
Limbu alijibu: “Nimeipata nimeona ni ndefu nimesoma kidogo na kuiweka kwenye gari hadi nitakapomaliza mkutano nitaisoma.”
Baada ya majibu hayo, Jaji Mutungi alimweleza Limbu kuwa akiisoma barua yake ataelewa alichokieleza.
Licha ya ufafanuzi huo, Limbu aliondoka eneo alilokuwa amesimama Jaji Mutungi huku akilalamika, lakini Msajili alinyamaza kimya bila kumjibu lolote na Mara kwa mara Limbu alionekana akimfuata Msajili alipokaa kwa kuendeleza malalamiko yake, lakini Msajili alionekana kuwa kimya.
MTANZANIA
Chama cha Wananchi (CUF), kimetangaza maandamano yanayofanyika leo jijini Dar es Salaam na kuongozwa na Waziri wa Miundombinu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Juma Duni Haji.
Duni ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, anatarajiwa kuwaongoza wafuasi wa chama hicho katika maandamao hayo licha ya Jeshi la Polisi kuyazuia.
Mbali ya Waziri Duni, maandamano hayo pia yataongozwa na viongozi wengine waandamizi wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa CUF (JUVCUF), Hamidu Bobali, alisema lengo la maandamano hayo ni kupinga uvunjwaji wa haki za binadamu na kuishinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), iongeze muda wa uandikishaji wapigakura.
Alisema hatua ya Jeshi la Polisi kutumia nguvu dhidi ya raia, inastahili kupingwa na kila mpenda amani kwani imekuwa ni mazoea yao kuwadhalilisha viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na raia pindi wanapokuwa katika maandamano.
MTANZANIA
Mahaakama ya Kazi Tanzania, Kitengo cha Usuluhishi na Uamuzi (CMA), jana imeipiga kalenda kesi inayomkabili aliyekuwa kipa wa Yanga SC, Juma Kaseja, hadi Machi 10 mwaka huu kutokana na nyaraka za upande wa walalamikiwa kuungua moto.
Kaseja alishtakiwa na timu yake hiyo ya zamani ikidai fidia ya Sh milioni 340, ambayo ni Sh milioni 40 pamoja na fidia ya Sh milioni 300, ambazo ni gharama za usumbufu wa kuvunja mkataba, kumhudumia na kutunza kiwango chake kwa kipindi chote alichokuwa Yanga.
Kesi hiyo ilianza kusikilizwa jana saa 5 asubuhi kwenye mahakama hiyo, kwa pande hizo mbili mbele ya Msuluhishi Fimbo, aliyesikiliza shauri hilo kwa niaba ya Masse aliyepata udhuru.
Kaseja alifika CMA na Mwanasheria, Mwenda Nestory, aliyemuwakilisha mwanasheria wake, Samson Mbamba, aliyepata udhuru, huku upande wa walalamikaji (Yanga) ukiwakilishwa na Mkuu wa Idara ya Sheria, Frank Chacha.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kusikilizwa shauri hilo, Chacha alisema shauri limeahirishwa baada yanyaraka za utetezi kwa upande wa walalamikiwa kuungua moto.
HABARILEO
Askari wa Jeshi la Polisi amejeruhiwa na madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda katika fujo zilizoibuka juzi jioni katika eneo la Mzinga, Kongowe Mbagala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam katika Manispaa ya Temeke.
Akizungumza kwa njia ya simu kuhusiana na tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Kihenye Kihenya alisema askari walikuwa kwenye doria kwa kutumia pikipiki maarufu kama Tigo na walipofika eneo la Mzinga walimkamata dereva mmoja aliyebainika kuwa na matatizo kadhaa kwenye pikipiki yake.
“Polisi walimkamata mwendesha pikipiki mmoja na ikabainika kwamba alikuwa na makosa kadhaa ambayo yalimpasa alipe faini. Lakini madereva wenzake walipoona amekamatwa wakaanzisha fujo na kumjeruhi mmoja wa askari kwa kumpiga chupa usoni:–Kihenya.
Aliongeza kuwa “Tumekamata bodaboda kumi na tano na tayari tunaendelea na uchunguzi ili kuweza kubaini wahusika wakuu na tuweze kuwafikisha mahakamani kwa kosa la shambulio,” alieleza.
HABARILEO
Siku chache baada ya Serikali kusema itazifutia usajili shule zitakazokaidi agizo la kuweka viwango maalumu na tofauti vya ufaulu kutoka kidato kimoja kwenda kingine, wadau wa elimu wamezungumza na kusema agizo hilo linalenga kuua ubora wa taaluma nchini.
Akizungumza na HabariLeo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo Visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Benjamin Mkoya alisema viwango vinavyowekwa na shule binafsi vinakubaliwa na wazazi na kuwa kinyume chake shule hizo zitakufa kutokana na uwezekano wa kufifia ubora wa kitaaluma.
“Viwango vinavyoweka huwa vinakubaliwa na wazazi, na lengo la kufanya hivyo ni kutaka shule zifanye vizuri hivyo kuweza kujiendesha, kwani mbali na kutoa huduma, tunafanya biashara:- Mkoya.
Alisema suala la baadhi ya shule kupanga viwango vya ufaulu limekuwa likifanyika muda mrefu na kuridhiwa na wizara husika ya elimu Julai 2013, baada ya agizo la kuifungia shule ya sekondari ya Mwilavya, Kasulu mkoani Kigoma iliyopandisha viwango vya ufaulu hadi kufikia asilimia 45 kutokana na matakwa ya wazazi.
Mkoya alisema suala hilo lilifika wizarani na uongozi wa TAMONGSCO kukutana na Naibu Waziri (wakati huo akiwa ni Philipo Mulugo) ambaye alisema kama wazazi wameridhia viwango hivyo, shule zinatakiwa kuendelea kufuata viwango hivyo.
MWANANCHI
Wakati serikali ikiongeza nguvu katika kupambana na utamaduni wa ukeketaji, Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) limesema idadi ya watoto chini ya mwaka mmoja wanaokeketwa imeongezeka kwa asilimia 10 nchini.
Akizungumza jana jijini hapa wakati Tanzania ilipokuwa ikitia saini mkataba wa kutokomeza ukeketaji na ndoa za utotoni, Mwakilishi wa UNFPA, Dk Natalia Kanem alisema vitendo hivyo vinafanywa na baadhi ya wahudumu wa afya.
“Mwacheni msichana atimize ndoto yake, mwambieni shikiria ndoto yako:- Dk Kanem.
Alisema lazima jamii kwa pamoja ishirikiane kuhakikisha wasichana wanatimiza ndoto zao za kuwa wanawake walio huru kutimiza malengo yao.
Balozi wa Uingereza nchini, Dianna Melrose alisema kitendo cha Tanzania kutia saini mkataba huo kimeonyesha kuwa Serikali imedhamiria kupambana na vitendo vinavyomnyanyasa mtoto wa kike.
“Kupiga vita ukeketaji na ndoa za utotoni kunampa fursa mtoto wa kike nafasi ya kumaliza masomo yake na pia mnaongeza idadi ya watoto shuleni:- Melrose.
MWANANCHI
Familia ya kijana Emmanuel Mpilla (27), aliyepoteza ndugu sita katika ajali ya moto, imepanga kumpa tiba ya kisaikolojia ili kuirudisha akili yake katika hali ya kawaida.
Mpilla alipoteza ndugu hao sita, akiwamo mama na baba yake, kaka yake, watoto wake wawili na mjomba wake katika tukio ya nyumba kuungua moto lililotokea usiku wa kuamkia Februari 7, Kipunguni A, Dar es Salaam.
Tangu kutokea kwa msiba huo, Mpilla hakutaka kuzungumza lolote, hali inayoonyesha ameathirika kisaikolojia.
Akizungumza kwa niaba ya familia, baba mkubwa wa Emmanuel, Merikioli Mpilla alisema uamuzi wa kumpa tiba ya kisaikolojia kijana huyo ulifikiwa katika kikao cha wanandugu kilichofanyika jana.
“Kuna mambo mengi ya kifamilia, tulipaswa tuyajadili, lakini kwa kifupi yanayomuhusu Emmanuel ndiyo yalitawala kikao:- Mpilla.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia Twitter, Instagram, na Facebook ukijiunga na mimi kwa kubonyeza >>>twitter Insta Facebook