Mabingwa wa Tanzania Azam Fc hii leo (jumapili) walianza vizuri kampeni yao katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika baada ya kushinda mchezo wao wa kwanza wa hatua ya awali ya michuano ya ligi ya mabingwa .
Azam imeshinda mchezo huo dhidi ya Al Mareikh ya Sudan kwa matokeo ya 2-0 katika mchezo uliopigwa huko Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam ukishuhudiwa na maelfu ya mashabiki waliojitokeza uwanjani humo kuishuhudia timu hiyo .
Azam walianza mchezo huo kwa kasi wakifunga bao la kwanza kwenye dakika ya 8 mfungaji akiwa mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi Didier Kavumbagu aliyemalizia krosi ya Brian Majwega ambayo iliambatana na kosa la beki wa Al Mareikh.
Baada ya hapo Al Mareikh walizinduka na kuanza kusambulia lango la Azam kwa kasi lakini hawakuweza kupata bao lolote huku mabeki wa mabingwa hao wa Tanzania na kipa Aishi Manula wakisimama vizuri na kuzia hatari zote zilizokuwa zinaelekea langoni .
Bao la pili la Azam lilikuja kwneye dakika ya 77 mfungaji akiwa John Bocco baada ya kufunga kwa kichwa akipokea pasi ya kichwa toka kwa Didier Kavumbagu ambaye aligusa mpira uliorushwa na Erasto Nyoni.
Azam walilazimika kufanya kazi ya ziada kwenye kipindi cha pili baada ya Al Mareikh kuwaingiza washambuliaji wake tegemeo Mohamed Traore na Augustine Okrah ambao waliongeza kasi ya mashambulizi.
Beki raia wa Ivory Coast Serge Paschal wawa hii leo alikuwa nyta wa mchezo baada ya kufanya kazi ya ziada ya kuokoa michomo iliyokuwa inaelekea langoni mwa Azam toka kwa washambuliaji wa Al Mareikh .
Timu hizi mbili zitarudiana wiki mbili zijazo huko nchini Sudan ambapo kama Azam wanahitaji kupata sare ya aina yoyote ile au kushinda ili kujihakikishia nafasi ya kufuzu hatua ya pili .